Raia 10, muasi wa ADF wauwa katika mapigano Beni
29 Machi 2018Vurugu hizo zilitokea siku ya Jumanne jioni wakati waasi waliposhambulia ngome za jeshi karibu na mji wa Beni, katika mkoa wa Kivu kaskazini, alisema Kapteni Mak Hazukay wakati akizungumza na shirika la habari la Ufaransa AFP. "Tumeonrodhesha maiti za raia 10 mpaka sasa," alisema.
Muasi kutoka kundi la Allied Democratic Forces (ADF), aliuawa pia, alisema, na kuongeza kuwa mapigano yalikuwa yakiendelea. Michel Kakule, daktari mkuu katika hospitali ya Beni, aliliambisha shirika la AFP kuwa baadhi ya waathirika, "walikuwa na majeraha ya risasi wakati wengine walishambuliwa kwa mapanga."
Shambulio hilo lilizusha hasira miongoni mwa wenyeji, "waliozuwia barabara kadhaa kuu katika mji huo kupiga mauaji ya raia 10," alisema Gilbert Kambale, anaefanya kazi na shirika la kiraia.
Tangu Januari, vikosi vya jeshi la Kongo vimeshiriki katika operesheni kubwa dhidi ya ADF lakini havijaweza kukomesha umuagaji damu ndani ya Beni na maeneo jirani.
"Kundi la ADF sasa linaendesha vita visopacha - tunapowashambulia katika eneo moja, wanajibu kwa kutushambulia kwingineko," alisema Hazukay. ADF ni moja ya makundi kadhaa ya silaha yanayoshikilia maeneo mashariki mwa DRC, ambayo yanapambana kudhibiti rasilimali za eneo hilo tajiri.
Kundi hilo la waasi, lilioundwa na Waislamu wenye itikadi kali waliokuwa wanapinga utawala wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni, limekuwepo Kivu Kaskazini tangu 1995 ambako linatuhumiwa kuuwa mamia ya raia katika kipindi cha miaka mitatu na nusu iliopita.
Limetuhumiwa pia kwa kuuwa wanajeshi 15 wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania, katika shambulio baya eneo la Beni Desemba mwaka uliopita.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/AFPE
Mhariri: Saumu Yusuf