Raia wa Guinea-Bissau Wapiga Kura Leo
13 Aprili 2014agombea 13 wanawania kiti cha Urais katika uchaguzi huu, na kila mmoja amewaahidi wananchi wa Guinea Bissau kwamba anao uwezo wa kusimama kidete mbele ya makamanda wa jeshi, na kulifanyia mageuzi jeshi mara tu atakapochaguliwa. Pia vyama 15 vinawania viti bungeni.
Kwenye mkesha wa uchaguzi huu, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, Kadre Desire Ouedraogo, amesema wagombea wote wamesema wamejitolea kwa dhati kujenga nchi mpya inayoheshimu sheria na uhuru wa watu.
Ouedraogo hali kadhalika amesema wagombea wote wameahidi kuheshimu na kukubali matokeo yatakayotangazwa.
Wanajeshi wako macho kuepusha ghasia
Uchaguzi huu ambao umeahirishwa mara kwa mara ni wa kwanza tangu Antonio Indjai aliyekuwa Mkuu wa Jeshi alipokubali kukabidhi madaraka kwa serikali ya mpito ya kiraia, iliyoongozwa na rais Manuel Serifo Nhamadjo, mwaka 2012.
Ingawa kipindi cha kampeni kilimalizika Ijumaa bila visa vikubwa vya fujo, uchaguzi huu unasimamiwa na wanajeshi 4,200 kutoka Guinea-Bissau na nchi nyingine za Afrika Magharibi. Wapo pia waangalizi zadi ya 500 wa kimataifa, ambao watatoa taarifa zao kuhusu iwapo uchaguzi huu umekuwa huru na wa kuaminika.
Kura ya leo inapigwa baada ya miongo minne ya ghasia zilizosababishwa na mlolongo wa visa vya uasi wa kijeshi, tangu Guinea-Bissau ilipopata uhuru wake kutoka Ureno. Wachambuzi wa masuala ya nchi hiyo wamekuwa wakiutolea wito utawala wa sasa kuweka nidhamu katika jeshi.
Suluhisho la mkwamo wa muda mrefu
Nchi hiyo maskini imekabiliwa na mkwamo mnamo miaka miwili iliyopita, chini ya utawala wa mpito unaoungwa mkono na jeshi, huku rushwa na uchuuzi wa madawa ya kulevya vikizidisha kusuasua kwa uchumi.
Mchambuzi mkuu wa Shirika la Kimataifa la Kushughulikia Mizozo, ICG, Vincent Foucher, amesema serikali itakayochaguliwa italazimika kuangalia upya marupurupu na upendeleo wanavyovipata maafisa wakuu jeshini, na kuanzisha upya mageuzi ambayo yalilichochea jeshi kufanya mapinduzi.
''Mara hii itabidi serikali iwe makini zaidi, na iwe tayari kutafuta maridhiano ili kuepusha ghasia nyingine za kijeshi.'' Amesema Foucher.
Muda mrefu wa ukosefu wa usalama umezidisha matatizo ya kiuchumi katika nchi hiyo yenye wakazi milioni 1.6, ambalo halina raslimali nyingi zaidi ya kilimo cha korosho na uvuvi. Umaskini huo umewarahisishia kazi walanguzi wa madawa ya kulevya kutoka Amerika ya Kusini kuigeuza Guinea Bissau kuwa kituo kikuu cha biashara yao katika ukanda wa Afrika Magharibi.
Shirika la Umoja wa Mataifa la viwango vya maendeleo limeiweka Guinea-Bissau katika nafasi ya 177 kati ya nchi 187, huku ikielezwa kuwa theluthi mbili ya wakazi wa nchi hiyo wako chini ya msitari wa umaskini.
Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE
Mhariri: Josephat Charo