1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Bongo wa Gabon ziarani Ujerumani

Lillian Urio17 Juni 2005

Rais Omar Bongo wa Gabon ni mmoja wa viongozi wa Afrika aliyekaa madarakani kwa kipindi kirefu. Rais Bongo, ambaye ametawala Gabon kwa miaka 38, sasa yuko Ujerumani kwa ziara ya siku tatu. Lengo kuu la ziara hii ni kutafuta wawekezaji kutoka Ujerumani, kwa ajili ya nchi yake iliyo katikati mwa Afrika.

https://p.dw.com/p/CHgQ

Rais Omar Bongo amezeeka na inambidi Rais huyo aongee taratibu na kwa kusitasita. Pia Rais huyo, mwenye miaka 70, anaonekana kama amechoka.

Akiongozana na mawaziri wake, Rais Bongo aliwasili katika kituo cha shirika la utangazaji la Ujerumani la Duetsche Welle, kuongelea juu ya ziara yake hapa Ujerumani.

Gabon inahesabika kama nchi iliyo na utulivu wa kisiasa barani Afrika, pamoja na kwamba nchi jirani ya jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo haina utulivu wa kisiasa kabisa.

Kabla ya hapo, Rais huyo wa Gabon alionana na kansela Gehard Schröder, wa Ujerumani. Katika ziara hii pia atakutana na Rais Köhler wa Ujerumani.

Mkutano ambao Rais Bongo anaungojea ni ule uliopangwa kufanyika katika mji wa Dresden, tarehe 17 mwezi huu, na wafanya biashara wa Ujerumani. Ambao wanafikra kwamba Afrika haifai kuwekeza.

Kwa maoni ya Rais Bongo hayo ni mawazo ambayo ni lazima yabadilishwe:

“Kansela wa Ujerumani na mimi tunawazo moja, kwamba inabidi tuongeze uhusiano wa kiuchumi. Na tumekubaliana kwamba, mawaziri wetu wa fedha, wakutane na wafanyabiashara wa Ujerumani walio na nia ya kuwekeza. Wataangalia rasilimali za kiuchumi za nchi yetu, yenye utajiri wa mali ghafi. Na kutokana na mazungumzo hayo wafanyabiashara wa Kijerumani wanaweza kuamua jinsi ya kuwekeza nchini Gabon”.

Pamoja na kuwa na mali ghafi, Gabon imekuwa ikijaribu kwa miaka mingi sasa, kukuza sekta ya utalii. Na katika sekta hii pia, Rais Bongo anataka kuwavutia wawekezaji.

Ingawa Gabon ina mali ghafi nyingi, zikiwemo mafuta na urani, ni mojawapo ya nchi maskini barani Afrika, ambayo itafaidika na maamuzi ya kundi za nchi za G7, ya kusamehe madeni.

Ufisadi na upendeleo wa kindugu katika ajira, unazuia faida za rasilimali hizo kunifaisha nchi nzima. Ndio maana nchi hiyo ina matatizo makubwa katika sekta za mawasiliano, afya na elimu. Ukosefu wa ajira unafikia asilimia 20.

Katika suala la biashara na nchi za nje, Ufaransa imetawala. Ndio maana, kupitia ziara hii, viongozi wa Gabon wanajaribu kuunda uhusiano na nchi nyingine.

Huu ni wakati ambapo kuna majadiliano mengi juu ya suala la kuleta mabadiliko barani Afrika. Mfano mpango wa kuleta maendeleo wa Waziri wa Fedha wa Uingereza, Gordon Brown. Au msamaha wa madeni ya nchi, ambayo Uingereza imesisitiza, kupitia kundi la nchi za G7. Lakini Rais Bongo anasema juhudi hizo hazitoshi:

“Kwa upande wake ni wazo zuri. Lakini mpango huu, uliopendekezwa na Waziri mkuu wa Uingereza, hatujaufurahia kabisa sisi Waafrika tulio katikati mwa bara, kabisa. Unozungumzia kuhusu Afrika nzima, kusini mwa sahara, lakini haitaji katikati mwa Afrika. Na katika nchi zitakazo samehewa madeni, hamna hata nchi moja kutoka katikati mwa Afrika. Tuaona kwamba G7 iongeze idadi za nchi. Gabon ni nchi ambayo sio tajiri wala sio maskini, iko katikati. Tuna matatizo sawa na nchi nyingine za Afrika, ukosefu wa ajira na umaskini. Na hatujaweza hatuja faidika na lolote. Kwa hiyo tumeadhibiwa, sababu hatujafaidika na msamaha wa madeni na pia wawekezaji wahawaji kwetu. Hayo yote yanazuia maendeleo ya Gabon”.

Rais Bongo hakutaka kuzungumzia kuhusu uchaguzi wa rais, utakaofanyika mwezi wa Desemba mwaka huu. Kiafya hakuonekana kama ana nguvu ya kuongoza kwa kipindi kingine kijacho, lakini suala la kuachi a madaraka lionaonekana kuwa gumu kwake na kwa wafuasi wake.