Rais Joseph Kabila atamchagua nani kugombea urais?
7 Agosti 2018Wanachama wa muungano wa vyama vinavyomuunga mkono rais Kabila unaojulikana kama Common Front for Congo (FCC) wameitwa kwenye mkutano huo muhimu jioni hii huko Kingakati, makao ya rais yaliyopo nje ya jiji la Kinshasa.
Chanzo kingine, cha karibu na rais Kabila, kimefahamisha kuwa hii sio siri tena- ni kuhusu kumtaja mgombea wa urais atakaye uwakilisha muungano wa vyama vinavyo muunga mkono kabila.Majina yanayovuma ni pamoja na waziri mkuu wa zamani Augustin Matata Ponyo, Mkuu wa shughuli za ikulu wa rais Kabila, Nehemie Mwilanya Wilondja na kiongozi wa Bunge la Kongo, Aubin Minaku.
Wagombea wana muda hadi kesho Jumatano saa12 na robo kwa saa za Afrika mashariki kuwasilisha makaratasi au fomu zao ushiriki katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe 23 mwezi Desemba 23.
Uchaguzi huo wa rais ulioahirishwa mara mbili unaonekana kuwa muhimu ufanyike kwa ajili kupatikana utulivu kwa nchi hiyo inayokumbwa na migogoro. Rais Joseph Kabila, ambaye amekuwa madrakani tangu mwaka 2001, alipaswa kuachia madaraka mwishoni mwa 2016 wakati muhula wake ulipofikia ukomo wake. Kwa mujibu wa katiba rais anastahili kuhudumu kwa kipindi cha mihula miwili.
Kabila amebadili kifungu cha katiba na hivyo kuwa na uwezekano wa kubaki madarakani kama mlezi wa taifa. Kiongozi huyo hadi sasa amemwacha kila mtu kwenye swali iwapo atagombea tena urais wan chi hiyo, labda kwa kufikiria kuwa hii inaruhusiwa kwa sababu ya marekebisho ya katiba mwaka 2006. Kutokuwa na uhakika kumeongeza mivutano ya kisiasa, inayosababisha maandamano ya kumpinga Kabila ambayo yamesababisha umwagikaji damu.
Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo nchi yenye watu milioni 80, haijawahi kushuhudia makabidhiano ya amani ya madaraka tangu ilipopata uhuru wake mwaka 1960. Rais Joseph Kabila, mwenye umri wa miaka 47, aliingia madarakani baada ya baba yake, Laurent-Desire Kabila, kuuawa mwaka 2001.
Utendaji kazi wake katika nchi hiyo kubwa yenye utajiri wa madini umekumbwa na sifa ya rushwa, kutokuwa na usawa na machafuko. Shirika la kimataifa linalopambana na rushwa la Transparency International limeiweka Kongo katika nafasi ya 156 kati ya nchi 176 zilizokithiri katika vitendo vya rushwa mnamo mwaka 2016.
Marekani iko tayari kuiwekea vikwazo zaidi Kjamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kumzuia Kabila kuendelea kushikilia madaraaka kwa nguvu. Marekani inajaribu kumshawishi Kabila aachie ngazi kati ya sasa na Agosti tarehe 8.
Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE
Mhariri:Iddi Ssessanga