Rais Kabila ahusishwa na mauaji ya Chebeya
17 Oktoba 2012Afisa aliyekuwa akihusika kuilinda nyumba alimouliwa mwanaharakati wa haki za binadamu Floribert Chebeya mwaka 2010 amezungumza na redio moja nchini Ufaransa na kudai kwamba rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Joseph Kabila alitoa amri ya kuuliwa mwanaharakati huyo.
Afisa huyo,Paul Mwilambwe anasema alishuhudia kuuwawa kwa Chebeya kupitia kamera ya uchunguzi.Afisa huyo hajulikani mahala aliko jificha barani Afrika lakini alizungumza kwa njia ya simu na redio ya Ufaransa RFI na kutoa madai hayo.
Mwilambe aliyetoroka mara tu baada ya kifo cha mwanaharakati huyo ni miongoni mwa maafisa wanne wa pamoja na kanali waliotuhumiwa kwa mauaji ya mwanaharakati huyo na walihukumiwa adhabu ya kifo bila ya wenyewe kuwepo mahakamani.Kwa maelezo aliyoyatoa kupitia Redio ya Ufaransa Mwilambe amesema aliwaona maafisa wa polisi katika kamera ya kunasa matukio,wakimbana pumzi kwa kutumia mfuko wa plastiki na gundi.
Afisa huyo pia amenukuu matamshi aliyoyasikia kutoka kwa bosi wake aliyesema kwamba alikuwa amepokea maagizo moja kwa moja kutoka kwa rais wa Jamhuri kupitia generali wa polisi John Numbi.Itakumbukwa kwamba Numbi alikuwa ni mtu muhimu katika Kongo akihusika na mazungumzo ya usuluhishi kati ya nchi yake na Rwanda.
Alitimuliwa baada ya kutokea mauaji hayo ya Chebeya,Mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu aliyekuwa na sifa kubwa na ambaye alikutwa ameuwawa ndani ya gari lake mnano mwezi Juni mwaka 2010.Alikuwa ni muasisi wa shirika la kutetea haki za binadamu likiitwa sauti ya wasiokuwa na sauti.
Inasaidikiwa kwamba kabla ya mauti kumfika alitoka pamoja na dereva wake kuelekea makao makuu ya polisi Kinshasa kwa ajili ya mkutano na bwana Numbi ambaye siku zote amekuwa akikanusha kuwahi kumuhoji Chebeya.Dereva wa Chebeya hajapatikana hadi hii leo.Madai ya Mwilambe yanasema kwamba amri iliyotolewa na rais Kabila iliwaamuru kumuua mtu yoyote aliyekuwa ameandamana na Chebeya siku hiyo.
Mauaji ya Mwanaharakati huyo yaliibua malalamiko na hasira katika Jumuiya ya Kimataifa na uchunguzi ukaanzishwa ambao hatimae uliwatia hatiani na kuhukumiwa kifo,Naibu kiongozi wa idara ya polisi ya masuala maalum,Kanali Daniel Mukalay,mnamo mwezi Juni mwaka 2011.
Maafisa wengine watatu wa polisi waliotoroka akiwemo Mwilambwe walipewa hukumu sawa na hiyo bila ya kuweko mahakamani na mwengine kuhukumiwa kifungo cha maisha gerezani na watatu wengine wakaondolewa mashtaka.Kesi nyingine ilitajwa mwezi Juni mwaka huu na inatarajiwa kuitishwa tena Oktoba 23.Watuhumiwa wanadai Numbi ndiye anayepaswa kuwa mshukiwa mkuu katika mauaji ya Chebeya na kudai achunguzwe upya.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Mohammed AbdulRahman