1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Kabila atarajiwa kumtangaza mrithi wake kuwania urais

8 Agosti 2018

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila anatarajiwa kumtangaza mgombea wa urais atakayemteua kupeperusha bendera ya muungano wa vyama vinavyomuunga mkono

https://p.dw.com/p/32nCJ
Joseph Kabila bei Rede 19.07
Picha: YouTube/CleboaPointCom News

Mgombea urais ambaye atapeperusha bendera ya muungano wa vyama vinavyomuunga mkono Joseph kabila katika uchaguzi ujao wa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC, atatangazwa leo. Hayo yamesemwa na msemaji wa rais Joseph Kabila.

Waziri mmoja aliliambia shirika la habari la AFP kuwa wanachama wa muungano unaomuunga mkono Joseph Kabila, ujulikanao kama Common Front for Congo (FCC), waliitwa katika makaazi ya rais viungani mwa mji wa Kinshasa jana jioni kwa kile kilichotajwa kuwa "mkutano muhimu.”

Msemaji wa rais Joseph Kabila, Lambert Mende ameliambia shirika la habari la AFP kuwa mgombea atakayeteuliwa atatangazwa mapema leo kufuatia mkutano huo wa jana.

Wanaopigiwa upatu kuteuliwa:

Baadhi ya majina yanayovuma kuwa huenda wakateuliwa kugombea urais kupitia muungano wa Kabila ni waziri mkuu wa zamani Augustin Matata Ponyo, Mkuu wa shughuli za ikulu ya rais Nehemie Mwilanya Wilondja na spika wa bunge Aubin Minaku.

Waziri Mkuu wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Augustin Matata Ponyo
Waziri Mkuu wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Augustin Matata PonyoPicha: AFP/Getty Images/J. D. Kannah

Wagombea wote wa urais wana hadi leo jioni kujaza na kuwasilisha fomu au nyaraka zao za kugombea urais katika uchaguzi huo utakaofanyika Disemba 23. Uchaguzi huo ambao umeahirishwa mara mbili, unatizamwa kuwa muhimu kwa mustakabali wa nchi hiyo ambayo mara nyingi si imara.

Waliohudhuria mkutano wa jana wamesema kuwa wakati wa mkutano huo rais Kabila aliwahutubia wale waliokuwepo, bila ya kujadili mustakabali wake mwenyewe kisiasa.

Kabila ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2001, alipaswa kuondoka madarakani mwaka 2016 wakati mihula yake miwili kikatiba ilimalizika. Lakini amekataa kusema ikiwa atagombea urais tena.

Hali ya wasiwasi kisiasa.

Baadhi ya washirika wake wanashuku huenda atajaribu kung'ang'ania madaraka na kugombea kwa muhula wa tatu licha ya kikomo cha kikatiba.

Hali hiyo ya kutokuwa na uhakika, imezidisha taharuki ya kisiasa nchini DRC, na kusababisha maandamano dhidi ya Kabila, maandamano ambayo wakati mwingine huzimwa kwa nguvu na kusababisha umwagikaji wa damu.

DRC ambayo ina watu milioni 80, haijawahi kushuhudia ukabidhiaji mamlaka kwa njia ya amani tangu ilipojinyakulia uhuru mwaka 1960.

Joseph Kabila alichukua uongozi kutoka kwa baba yake, Laurent Desire Kabila ambaye aliuawa na mlinzi wake.

Miongoni mwa wale ambao wameshajiandikisha kugombea urais ni kiongozi wa zamani wa waasi Jean pierre Bemba