Rais wa Kongo afanya mabadiliko makubwa jeshini
20 Desemba 2024Amri ya rais iliyosomwa kupitia kituo cha televisheni ya taifa haikueleza sababu ya kuondolewa kwa mkuu huyo ya majeshi Christian Tshiwewe Songesha, na nafasi yake kuchukuliwa na Luteni Jenerali Jules Banza Mwilambwe.
Wataalamu wa masuala ya jeshi na ulinzi wanadhani, kwamba kuteuliwa kwa Luteni Jenerali Banza Mwilambwe Jules, anaetokea kwenye kikosi cha ulinzi wa rais, kama mtangulizi wake, huenda hapatakuwa na mafanikio zaidi kwenye vita vinavyoendelea mashariki mwa nchi hiyo kwa zaidi ya miaka miwili sasa.
"Lazima kuweko na maboresho"
Kuna wale wanaodhani kwamba, mabadiliko stahiki, ni yale yanayoanzia kwenye ngazi za chini na kupanda juu, kama anavyosema Patrick Mundeke, mwanasiasa na pia mchambuzi wa masuala ya ulinzi.
"Ilikutegemea mabadiliko kwenye uwanja wa mapigano, lazima kuweko na maboresho ya hali ya maisha ya wanajeshi, kuweko na uongozi wa jeshi ulionawatu wenye uzoefu.", alisema Mundeke.
Kwa upande wake Marrion Ngavo, mwenyekiti wa mashirika ya kiraia katika mji wa Goma, amepongeza mageuzi hayo ya jeshi, huku akiwaomba viongozi wapya wa jeshi, kuyarejesha chini ya udhibiti wa jeshi maeneo yaliyotekwa na waasi wa AFC-M23.
Ifahamike kuwa, mabadiliko katika uongozi wa jeshi yanafanyika, wakati waasi wa AFC-M23, wanaonekana kusonga mbele kwenye uwanja wa mapambano, katika wilaya ya Lubero, eneo la kaskazini la mkoani wa Kivu Kaskazini.
Juhudi za upatanishi zaendelea
Wakati huohuo, jopo la kimataifa la wadau wa nchi za ukanda wa maziwa makuu, linaloongozwa na Uholanzi, limetangaza kusikitishwa kufuatia kusuasua kwa mazungumzo ya Luanda, baina ya Rwanda na Kongo.
Katika tamko lao la pamoja lililotolewa Alhamisi, jopo hilo limewaomba viongozi wa Kongo na Rwanda kurudi kwenye meza ya mazungumzo, ili kufanikisha amani ya kudumu katika mkoa wa Kivu Kaskazini, ambao umegeuka kuwa uwanja wa mapigano.
Aidha jopo hilo linalowaleta pamoja wajumbe kutoka Ubelgiji, Umoja wa Ulaya, Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi, Sweden, Uswisi, Uingereza na Marekani, lilimpongeza rais wa Angola João Lourenço, kwa jitihada zake, ilikuwaleta pamoja kwa mazungumzo, viongozi wa Rwanda na Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.