1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa nchi za ASEAN na Marekani wakutana Malaysia

Admin.WagnerD20 Novemba 2015

Rais wa Marekani Barack Obama amewasili nchini Malaysia leo hii, kwa lengo la kuhudhuria mkutano wa viongozi wa nchi na serikali za jumuiya ya nchi za Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN).

https://p.dw.com/p/1H9ML
Malaysia ASEAN Außenministertreffen in Kuala Lumpur
Picha: Reuters/B. Smialowski

Obama atajiunga pamoja na viongozi wengine 10 wa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo ya ASEAN kwa mazungumzo ya siku mbili za mwisho wa wiki. Viongozi wa nchi nyengine saba - Australia , China, India, Japan, New Zealand, Urusi na Korea Kusini- pia watahudhuria mfululizo wa mikutano itakayoanza kesho.

Usalama umeimarishwa katika mji mkuu wa nchi hiyo Kuala Lumpur baada ya kutokea mashambulizi ya kigaidi mjini Paris Ijumaa iliyopita pamoja na kuangushwa kwa ndege ya Urusi na wanamhambo wa kundi la dola la kiislamu IS nchini Misri.

Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo ya Nchi za Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN) amesema wanaziunga mkono jitihada za kukabiliana na ugaidi.

Le Luong Minh ASEAN Generalsekretär
Le Luong Minh, Katibu Mkuu wa jumuiya ya ASEANPicha: AFP/Getty Images/K. Nogi

"Katika kila mkutano wa kilele wa ASEAN tumekuwa tukielezea misimamo yetu pamoja na wasiwasi wetu juu ya matukio kama haya mashambulizi ya hivi karibuni ya kundi la IS nchini Ufaransa pamoja na Lebanon, na nataka kusisitiza kwamba ASEAN iko pamoja na suala la kupambana na ugaidi," alisema Le Luong Minh, katibu mkuu wa jumuiya hiyo.

Mkuu wa vikosi vya jeshi Zulkifeli Mohd Zin amesema takriban wanajeshi 2,000 wamesambazwa katika maeneo mbalimbali mjini Kuala Lumpur huku wengine 2,500 wakiwa wamewekwa tayari iwapo kutahitajika usalama zaidi.

Obama pamoja na viongozi wengine kadhaa wamewasili nchini Malaysia wakiwa wanatokea kwenye mkutano mwengine wa kilele wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Marekani na Asia APEC uliofanyika mjini Manila, Ufilipino ambapo rais huyo wa Marekani alijaribu kuishinikiza China juu ya hatua zake za kutaka kudhibiti maeneo kadhaa kwenye bahari ya kusini mwa China.

Katika mazungumzo na Rais wa Ufilipino siku ya Alhamisi Obama aliitaka China kusitisha hatua zake zote za kuokoa ardhi na kujenga visiwa katika mwamba wa bahari ya kusini mwa China.

Ingawa nchi wanachama wa ASEAN zinatarajiwa kuchukua msimamo wa pamoja kuhusu shughuli za China katika eneo hilo la Bahari ya Kusini mwa China, Katibu wake Mkuu amesema kuwa hashangazwi na uamuzi wa nchi wanachama wa muungano huwo wa kutaka mgogroro utatuliwe kwa njia za amani.

Mikutano hiyo ya kilele ya APEC na ASEAN kawaida huzingatia masuala ya kiuchumi mara hii imegubikwa na jitihada za kimataifa za kupambana na kundi la dola la Kiislamu IS kufuatia mashambulizi ya mjini Paris yaliyosababisha vifo vya watu 129.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre

Mhariri: Yusuf Saumu