1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini kujiuzulu

Mohmed Dahman20 Septemba 2008

Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini amekubali kujiuzulu baada ya chama tawala cha ANC kumtaka ajiuzulu.

https://p.dw.com/p/FLwo
Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini.Picha: picture-alliance /dpa

Uamuzi huo wa chama cha ANC wa kumuondowa Mbeki ambaye amekuwa akipendwa na wawekezaji kutokana na sera zake zenye kupendelea biashara kunaweza kusababisha ukosefu wa utulivu wa kisiasa katika nchi hiyo yenye nguvu kubwa kabisa za kiuchumi barani Afrika ikiwa ni miaka 14 ya baada ya kuondokana na utawala wa ubaguzi wa arangi.

Katika taarifa ofisi ya rais imesema kufuatia uamuzi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama cha ANC kumtaka Mbeki ajiuzulu Rais amekubali na atajiuzulu baada ya kutimizwa kwa matakwa yote ya katiba.

Katibu Mkuu wa chama cha ANC Gwede Mantashe alitangaza uamuzi huo wa chama cha ANC kwa waandishi wa habari mjini Johannesburg leo hii.

Mantashe amesema baada ya majadiiano marefu na magumu chama cha ANC kimeamuwa kumtaka rais ajiuzulu kabla ya muda wake kumalizika na kwamba amejulishwa uamuzi huo.

Uamuzi huo hivi sasa lazima uidhinishwe na bunge jambo ambalo litakuwa ni kama taratibu tu kwa kuzingatia kwamba chama cha ANC kina wingi wa viti wa theluthi mbili bungeni.

Mbeki ambaye ameitawala Afrika Kusini tokea Mzee Nelson Mandela alipostaafu hapo mwaka 1999 alikuwa akitazamiwa kuondoka madarakani hapo mwaka 2009.

Mwaka jana alipoteza uongozi wake wa chama kwa Jacob Zuma.

Zuma ambaye ni mashuhuri kwa wafuasi wa sera za mrengo wa shoto na vyama vya wafanyakazi na washirika wao wa kikomunisti anawekewa matumaini makubwa ya kurithi nafasi ya Mbeki.

Kamati ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho cha ANC ambacho ni chombo cha juu cha maamuzi cha chama hicho kimeamuwa kumtaka Rais Mbeki ajiuzulu kufuatia miaka kadhaa ya malumbanoo ndani ya chama tokea uamuzi wake wa kumtimuwa naibu wake wakati huo Jacob Zuma hapo mwaka 2005.