Rais Zelensky wa Ukraine ana amini Urusi itashindwa
21 Agosti 2023Rais Zelensky ameyasema hayo leo Jumatatu katika hotuba aliyoitowa nje ya bunge la Uholanzi na kushangiliwa na umati wa watu huku wakipeperusha bendera za Ukraine. ''Tunausubiri huo wakati,utakuwa ni ushindi wa pamoja ,ushindi kwa demokrasia,kwa watu wetu na mataifa yetu.Asanteni sana kwa uungaji mkono wenu'' Hotuba ya kiongozi huyo wa Ukraine imekuja siku moja baada ya Denmark pamoja na Uholanzi kutangaza kuwa tayari kuipatia nchi hiyo madege ya kivita aina ya F-16 yaliyotengenezwa Marekani ili kuliimarisha jeshi lake la wanaanga la tangu enzi ya muungano wa Kisovieti.Waziri Mkuu wa Denmark Mette Frederiksen alitangaza hapo jana kuwa tayari kuipelekea ndege hizo 19 kwa Ukraine, sita kati ya hizo zitapelekwa kufikia mwisho wa mwaka huu. Hivi leo, Urusi imetoa tahadhari juu ya kitendo hicho cha kuipelekea Ukraine madege hayo ya kivita ikisema ni kitendo kinachochochea zaidi vita.