1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBolivia

Rais wa Bolivia akanusha kuhusika na jaribio la mapinduzi

28 Juni 2024

Rais wa Bolivia Luis Arce amekanusha kuhusika na jaribio la mapinduzi dhidi yake. Amesema kamanda aliyeliongoza jaribio hilo alilifanya mwenyewe. Watu 17 wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

https://p.dw.com/p/4hc8p
Bolivien Putschversuch gescheitert | Präsident Luis Arce
Picha: Josue Cortez/REUTERS

Katika hotuba yake ya kwanza mbele ya waandishi wa habari tangu jaribio hilo la mapinduzi lililoshindwa, Arce alisema madai kuwa alijipangia mapinduzi ni uwongo, akiongeza kuwa yeye sio mwanasiasa anayetafuta uumarufu kupitia damu ya watu.

Arce alizungumza saa kadhaa baada ya serikali yake kutangaza kuwa jumla ya watu 17 wamekamatwa kwa kuhusika katika jaribio hilo la kuiangusha serikali, akiwemo mkuu wa majeshi, Jenerali Juan Jose Zuniga, na Kamanda wa zamani wa Jeshi la Wanamaji Juan Arnez Salvador.

Rais Arce alidai kuwa sio tu maafisa wa kijeshi walihusika katika mpango huo, lakini watu waliostaafu kutoka jeshini na mashirika ya kiraia. Hata hivyo hakufafanua madai hayo. Amesema Zuniga atachunguzwa na kukabiliwa kisheria. Hapo jana baadhi ya wafuasi wa rais huyo walifanya maandamano nje ya ikulu kuonesha uungwaji mkono.