Rais wa Comoro amesitisha korti ya katiba
20 Aprili 2018Rais wa Comoro amesitisha korti ya katiba, mahakama ya juu kabisa katika taifa hilo la visiwa katika bahari ya Hindi, katika hatua ambayo ilikosolewa mara moja na upinzani. Rais Azali Assoumani amesema mahakama hiyo ilikuwa haifanya kazi kutokana na idadi ya majaji walioteuliwa kutokuwa kamili.
Uamuzi wa rais ulipitishwa Aprili 12 lakini ukatangazwa wiki hii. Comoro, taifa la visiwa kati ya Msumbiji na Madagascar na mojawapo ya mataifa maskini kabisa duniani, limekabiliwa na ukosefu wa uthabiti na migogoro ya kisiasa kwa miaka kadhaa.
Assoumani, aliyeingia madarakani mwaka 2016 kwa awamu yake ya tatu, amesema mahakama ya juu kabisa itachukua majukumu ya korti ya katiba kwa muda.
Chama cha upinzani Union for the Development of Comoros, UPDC, kimesema hatua hiyo ni matumizi mabaya ya madaraka na kwamba Rais Assoumani kwa makusudi alichelewesha uteuzi wa majaji wa korti ya katiba.