1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hatimae rais Joe Biden wa Marekani anakwenda Angola

1 Desemba 2024

Joe Biden ni rais wa kwanza wa Marekani kuitembelea Angola tangu ilipopata Uhuru 1975 kutoka kwa Wareno.

https://p.dw.com/p/4ncNH
Rais Joe Biden akiwa na mwenzake Joao Manuel Lourenco wa Angola, mjini Washington
Rais Joe Biden na mwenzake Joao Manuel Lourenco wakizungumza WashingtonPicha: Yuri Gripas/ABACAPRESS/picture alliance

Rais anayeondoka madarakani nchini Marekani,Joe Biden anaanza ziara yake nchini Angola kuanzia Jumatatu, akitimiza ahadi muhimu aliyoitowa 2022 ya kuimarisha mahusiano na bara la Afrika kwa kuitembelea nchi hiyo.

Biden atakaa mjini Luanda, mji mkuu wa Angola, kuanzia Jumatatu hadi Jumatano ,akiwa rais wa kwanza wa Marekani kuitembelea nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika yenye utajiri wa mafuta,tangu ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Wareno mwaka 1975.

Akiwa Angola anataka pia kuimarisha uwepo wa Marekani katika bara hilo katika kiwingu cha kuongezeka kwa uwekezaji unaofanywa na China.

Joe Biden, Joao Lourenco, Xi Jinping
Joe Biden, Joao Lourenco, Xi JinpingPicha: IMAGO/Getty Images/picture alliance

Rais Biden ambaye kwa sasa hana maamuzi makubwa, wakati anajiandaa kumkabidhi madaraka Donald Trump Januari 20, alipanga mwazoni kufanya ziara yake hiyo mwezi Oktoba lakini ilisogezwa mbele kutokana na kimbunga Milton kilichopiga katika jimbo la Florida.

Hata hivyo afisa mmoja mwandamizi katika serikali ya Marekani amesema ziara hii ya Biden bado haijachelewa.Soma pia: Blinken kuzuru Afrika wakati mizozo ikiendelea kutatiza sera ya kigeni ya Marekani

Yatakayojadiliwa Luanda

Rais Biden atajadili kuhusu masuala mbali mbali ya uwekezaji akiwa mjini Luanda,ikiwemo mradi wa mkubwa wa reli wa Lobito,ambao unahusisha ujenzi wa reli hiyo inayounganisha bandari ya Agola ya Lobito hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,ikiunganisha hadi Zambia.

Mradi huo wa ujenzi wa kilomita 1,300 umegharimiwa na Marekanii pamoja na Umoja wa Ulaya na umetajwa na rais Biden kama ndio uwekezaji mkubwa wa reli barani Afrika kuwahi kufanyika.Soma pia: Angola, DRC zalenga ukarabati wa reli muhimu kukidhi kiu ya madini duniani

Luanda,Angola
Mji mkuu Luanda,AngolaPicha: José Adalberto/DW

Mradi huo wa kimkakati unaiunganisha bandari na migodi ya Kobalti na shaba,madini muhimu katika utengenezaji wa betri za simu za mkononi za kisasa pamoja na utenezaji wa bidhaa nyingine za kiteknolojia.

Atakuwa na mkutano na rais Joao Lourenco wa Angola  na kutowa hotuba kuhusu masuala ya afya ya umma,kilimo,ushirikiano wa kijeshi na uhifadhi wa urithi wa kitamaduni.

Lakini pia mashirika ya kutetea haki za binadamu yametowa mwito kwa rais huyo wa Marekani kulizungumzia suala la rekodi mbaya ya Angola ya haki za binadamu katika ziara yake hii.

Kwa mujibu wa ripoti za hivi karibuni za Amnesty International,Polisi  wa Angola wamehusika katika mauaji ya takriban waandamanaji  17 ikiwemo wa umri mdogo,katika harakati zao za kuwaandama wapinzani

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW