1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa mpito aapishwa Gabon

Oumilkher Hamidou10 Juni 2009

Mwenyekiti wa baraza la senet bibi Rogombé akabidhiwa hatamu za uongozi

https://p.dw.com/p/I6xr
Rais Bongo (kushoto) akizungumza na rais wa Ufaransa Jacwues Chirac (kati) na rais Sassou NgwessouPicha: picture-alliance/ dpa/dpaweb

Siku mbili baada ya kufariki dunia rais wa Gabon,El Haj Omar Bongo nchini Hispania,mwenyekiti wa baraza la Senet ,bibi Rose Francine Rogombé ameapishwa hii leo kua rais wa muda nchini humo.Maiti ya rais Bongo inatazamiwa kurejeshwa nchini kesho na maziko yake yatafanyika June 18 ijayo.

Kabla ya mwenyekiti wa baraza la Senet kuapishwa,mwenyekiti wa baraza la katiba bibi Marie-Madeleine MBORANTSOUO aliwaomba wote waliohudhuria hafla hiyo katika ukumbi wa mkutano wa jengo la demokrasia, wakiwemo wabunge,maseneta,waziri mkuu na serikali yake na mabalozi waliko mjini Libreville wakae kimya kwa dakika moja kumkumbuka rais Bongo ambae habari za kifo chake zilitangazwa jumatatu iliyopita mjini Barcelona nchini Hispania.

Kuambatana na katiba ya Gabon,mwenyekiti wa baraza la Senet ndie anaestahiki kukabidhiwa hatamu za uongozi wa taifa pindi rais akishindwa kuendelea na wadhifa wake.

Mtaalam wa masuala ya sheria kutoka Gabon,Rufin Nkounlou anadhibitisha kwa kusema:

"Kifungu nambari 13 kinazungumzia juu ya hatua kadhaa zinazostahiki kuchukuliwa ili kumuwezesha mwenyekiti wa baraza la senet akabidhiwe wadhifa wa rais wa jamhuri."

Mwenyekiti wa baraza la Senet,bibi Rose Francine Rogombe mwenye umri wa miaka 66,ameahidi kuwajibika ipasavyo,mbele ya taifa na raia,kuheshimu na kuilinda katiba na kuendeleza dola linaloheshimu sheria.

Hafla hiyo imefanyika katika ukumbi ule ule alikoapishwa marehemu rais Bongo,January 19 mwaka 2006, baada ya kuchaguliwa kwa kipindi chengine cha miaka sabaa,November mwaka 2005.

Bibi Rogombé atakua na madaraka yote ya rais isipokua haruhusiwi kuitisha kura ya maoni wala kulivunja bunge.

Kwa mujibu wa katiba rais wa muda anabidi aitishe uchaguzi wa rais,siku 45 baada ya kuapishwa.

Regenwald mit Elefant in Gabun Afrika
Ardhi ya rutuba na misitu ya joto ya GabonPicha: AP

Hata hivyo mwenyekiti wa baraza la katiba,Marie-Madeleine Mborantsouo amezungumzia uwezekano wa kurefushwa muda wa rais wa mpito ikihitajika.

Wakatai huo huo serikali ya Ufaransa,mtawala wa zamani wa kikoloni nchini Gabon,na mshirika mkubwa wa rais aliyefariki dunia Omar Bongo,inasema "itaendelea kuwaunga mkono wananchi wa Gabon na taasisi zake bila ya kuupendelea upande wowote.Hayo ni kwa mujibu wa waziri wa ushirikiano Alain Joyandet alipoulizwa na waandishi habari kama wanamuunga mkono au la mtoto wa kiume wa rais Bongo Ali Ben Bongo anaetajikana kua na nafasi nzuri ya kumrithi babaake.

Na hayo yakiendelea maiti ya rais Bongo inatazamiwa kuwasili mjini Libreville kesho jioni.Mazishi yake yatafanyika June 18 ijayo huko Franceville katika jimbo alikozaliwa la Ogooué.




Mwandishi :Oummilkheir Hamidou/AFP

Mhariri:M.Abdul-Rahman