Raul kuihama Schalke mwisho wa msimu
20 Aprili 2012Raul mwenye umri wa miaka 34 ambaye aliwahi kuichezea Real Madrid ya uhispania amekuwa katika klabu ya Schalke kwa misimu miwili, huku akifunga magoli 27 ya Bundesliga katika mechi 63. vyombo vya habari vya Ujerumani vilisema kuwa Raul huenda akaendelea na taaluma yake Qatar.
Mchezaji huyo aliwaambia waandishi habari kuwa maisha yake ya usoni yako nje ya ulaya katika ligi ambayo sio imara sana kimchezo kama vile Bundesliga. Alisema umekuwa uamuzi mgumu kufanya, akiongeza kuwa ataiweka klabu ya Schalke moyoni mwake.
Robben azozana na Ribery
Gazeti la Ujerumani la Sport Bild limeripoti kuwa mchezaji Arjen Robben amekataa uhamisho wa kujiunga na klabu ya Juventus kutoka Bayern Munich, licha yeye kuwa na mzozo na mwenzake Franck Ribery.
Gazeti hilo limeripoti kuwa wachezaji hao wawili walihusika katika mzozo mkali wakati wa mapunziko baada ya kipindi cha kwanza cha mchuano wao wa ligi ya mabingwa dhidi ya Real Madrid. Gazeti la Ujerumani la Sport Bild limeripoti kuwa mgogoro huo ulihusu ni nani aliyefaa kuipiga free kick pembeni mwa eneo la hatari muda mfupi kabla ya kipindi cha mapumziko.
Gazeti la Bild pia lilionyesha shavu lililochibuka la Robben na likadai kuwa huenda lilisababishwa na ngumi iliyopigwa na Ribery. Klabu ya Bayern ilikataa kuzungumzia suala hilo. Msemaji wa klabu hiyo Markus Horwick alisema kile kinachofanyika katika chumba cha wachezaji kuvalia nguo uwanjani kinasalia huko.
El-Classico ya sita
Mahasimu wawili wakali Barcelona na Real Madrid watakutana Jumamosi katika pambano la sita maarufu kama el classico msimu huu ili kung'ang'ania pointi tatu muhimu ambazo zitatoa mwelekeo wa hatima ya taji la ligi kuu ya soka Uhispania - La Liga.
Huku kukiwa na mechi tano zilizosalia msimu kukamilika, Real Madrid watakwenda Nou Camp wakiwa na faiday a pointi nne kileleni mbele ya mahasimu wao wakuu wakifahamu kuwa ushindi au sare utawahakikishia vijana hao wa Jose Mourinho ubingwa wa taji hilo na kuwapokonya Barcelona kombe. Mourinho huenda akawapumzisha baadhi ya wachezaji wake wa kila mara kabla ya mchuano wa marudiano Bayern.
Ushindi wa Real katika fainali ya msimu uliopita ya Kombe la Mfalme maarufu kama Copa del Rey ulidhihirisha kuwa vijana wa Mourinho wanaweza kuwashinda Barcelona baada ya majaribio matano yaliyogonga mwamba.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters/dpa/ap
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman