RB Leipzig kuonja joto la Champions League
13 Septemba 2017Washambuliaji Neymar, Kylian Mbappe walionunuliwa na klabu hiyo kwa kitita cha juu kabisa pamoja na Edson Cavani kila mmoja alipachika mabao mawili.
Messi wa Barcelona na Robert Lewandowski wa Bayern Munich nao pia walionesha umahiri wao wa kupachika mabao. Huo ulikuwa mwanzo wa msimu mpya wa kinyang'anyiro cha kombe la mabingwa barani Ulaya. Leo hii michuano hiyo inaendelea kwa michezo mingine minane.
RB Leipzig inayodhaminiwa na kampuni inayotengeneza kinywaji cha kuongeza nguvu mwilini Red Bull , inajitupa uwanjani jioni ya leo ikijaribu kwa mara ya kwanza kuangalia hali ya hewa katika anga hizo za juu katika soka la Ulaya ikipambana na AS Monaco ya Ufaransa.
RB Leipzig iko tayari kwa Champions League, lakini Champions League iko tayari kwa Leipzig ? Hilo ni swali la dola milioni mbili. Ikija katika kuorodhesha timu ambazo zinauwezo wa kunyakuwa kombe hilo , kwa kawaida majina makubwa ndio hutajwa , lakini hakuna mtu atakayeitaja RB Leipzig katika orodha hiyo. Je hilo litakuwa kosa kubwa ? mashabiki wa Ulaya na duniani kwa jumla jioni ya leo watapata fursa ya kuangalia kwa karibu kikosi kinachopewa mafunzo na kocha raia wa Austria Ralph Hasenhuettl.
Borussia Dortmund
Borussia Dortmund inaingia uwanja wa Wembley leo jioni ikiwa na kumbukumbu ya kutoka patupu katika fainali ya Champions League mwaka 2013 dhidi ya Bayern Munich , licha ya kwamba mara hii inacheza na timu kutoka Uingereza Tottenham Hot Spurs na sio katika fainali bali ni mchezo wa kwanza wa kundi H. Mchezo mwingine wa kundi H unazikutanisha Real Madrid ambao ni wenyeji wa pambano lao dhidi ya APOEL Nicosia ya Cyprus.
Liverpool ya Uingereza nayo imerejea katika kinyang'anyiro hicho na kocha Juergen Klopp anahaja ya kuonesha kwamba kufika fainali mwaka 2013 akiwa na Borussia Dortmund ya Ujerumani haikuwa jambo la kubahatisha.Liverpool inaonshana kazi na Seville ya Uhispania.
Kocha mwenye mafanikio makubwa katika soka barani Ulaya Pep Guardiola anajaribu mitambo yake tena mara hii akiwa na Manchester City akikabiliwa na Fayenoord ya Uholanzi. Napoli ya Italia itakuwa nchini Ukraine ikiumana na Shakhtar Doneszk. Porto ya Ureno ina miadi na Besiktas ya Uturuki na Maribor ya Slovenia inapambana na Spartak Moscow ya Urusi.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe
Mhariri: Idd Ssessanga