1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Robben na Lahm warejea katika Bayern

20 Desemba 2016

Arjen Robben na Philip Lahm wataungana na wenzao kwenye kikosi cha Bayern Munich wakati vinara hao wa ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga wakiwakaribisha mahasimu wao RB Leipzig wanaoshikilia nafasi ya pili

https://p.dw.com/p/2Ubx6
UEFA Champions League FC Bayern München vs. Club Atletico de Madrid
Picha: Getty Images/Bongarts/M. Hitij

Leo hii kocha Carlo Ancelotti wa Bayern Munich amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari kwamba wachezaji hao wako fiti na hawana tatizo lolote, na watapewa nafasi kubwa ya kujiunga kwenye kikosi kitakachocheza Jumatano. Kinyume na hapo mlinzi wa kikosi hicho Jerome Boateng atakuwa nje kwa takriban wiki sita baada ya kufanyiwa upasuaji wa kifua, na anatarajiwa kurejea uwanjani mwezi Februari.

Ancelotti amesema mechi hiyo itakuwa ni mchezo wenye mvuto kwa yoyote anayependa soka na kusisitiza kwamba anachohitaji ni Bayern  kuchukua pointi zote tatu, ingawa hata droo bado inawahakikishia kusalia kileleni mwa ligi kutokana na tofauti ya magoli kati yake na Leipzig. 

Baada ya mchezo huu, Bundesliga inasimama kwa ajili ya mapumziko ya kipindi cha baridi, hadi mwishoni mwa mwezi Januari mwakani, itakaporejea tena.

Kwenye mchezo wake wa mwisho, Jumapili iliyopita Bayern Munich iliondoka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya timu iliyoko miongoni mwa zinazoburuza mkia za Bundesliga ya Darmstadt. Alikuwa ni Douglas Costa aliyefunga bao hilo pekee.

Fußball Bundesliga FC Schalke 04 - RB Leipzig
Wachezaji wa Leipzig walipokutana na Schalke 04Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Meyer

Bayern wanakutana na Leipzig ambayo hadi sasa imefungwa mechi moja tu, na hivyo kukitarajiwa kuwepo na ushindani mkali. "Kesho tutaona wapinzani hao wawili wakicheza kwa mtindo tofauti" amesema Ancelotti. Tutasalia kwenye mtindo wetu na kujipanga. Tutahakikisha tunaimarisha safu yetu ya ulinzi.

"Kitu muhimu kwa ushindi wa kesho ni kuhakikisha kunakuwepo na usawa kati ya safu ya ulinzi na mashambulizi, aliongeza. Mashabiki takriban 75,000 wanatarajiwa kuwepo ndani ya uwanja wa Alianz Arena kushuhudia mchezo huo. 

Kwa upande wa Leipzig, mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo Ralf Rangnick naye amesema anachohitaji ni timu hiyo kunyakua pointi zote tatu kwenye mchezo huo, pamoja na kuamini kwamba timu yake bado ina safari ndefu kama ina nia thabiti ya kuwa mpinzani halisi wa Bayern Munich.

Bayern na Leipzig zinakutana zikiwa zimefungana kwa pointi, na Rangnick nae haonyeshi kukata tamaa na kuendelea kujizatiti katika kinyang'anyiro hicho cha kuwania ubingwa wa Bundesliga. 

Rangnick amesema Bayern inabaki kuwa timu yenye mafanikio makubwa zaidi, tofauti na Leipzig ambayo inachukiwa na mashabiki wengi wa Ujerumani kutokana na ufadhili mkubwa wa kifedha inayopata kutoka kwa kampuni ya kinywaji cha kuongeza nguvu cha Red Bull. Wanaiita klabu hiyo kuwa ni feki, wakiifananisha na klabu nyingine kama Bayer Leverkusen, Wolsburg na Hoffenheim.

Mwandishi: Lilian Mtono.
Mhariri:  Iddi Ssessanga