Robert Lewandowski haendi Bayern mwaka huu
10 Juni 2013Kumekuwa na uvumi kuwa mshambuliaji huyo raia wa Poland analenga kujiunga na mabingwa hao wa Ujerumani na Ulaya. Gazeti la BILD limemnukuu Watzke akisema „Robert Lewandowski hatasaini mkataba na Bayern Munich mwaka wa 2013“. „Hiyo ni kauli ya mwisho, na tumemwambia Robert na wakala wake.“ Watzke amesema wachezaji wako huru kuzungumzia matukio ya uhamisho, na kwamba yeye binafsi alifanya mazungumzo mara mbili na Bayern.
Dortmund waliwaambia mahasimu wao Bayern kuwa walitarajia kupokea ombi rasmi la kumtaka Lewandowski kwa njia ya maandishi, lakini hakuna chochote kilichowasilishwa. Hivyo basi suala hilo limekamilika, na kama Robert atataka kujiunga na Bayern, basi atafanya hivyo mwaka ujao.
Lewandowski mwenye umri wa miaka 24 aliliambia gazeti la BILD mapema mwezi huu kuwa alitaka kiondoka Dortmund kabla ya kunza msimu mpya, ijapokuwa hakuitaja klabu ya Bayern. Kama Lewandowski ataondoka mwaka ujao, Dortmund itapata hasara, kwa sababu Mpoland huyo hatakuwa na mkataba, hivyo Bayern, au klabu nyingine yoyote inaweza kupata huduma zake bila malipo yoyote kwa BVB.
Na tukisalia na suala hilo la Bayern, mchuwano wa kirafiki wa kabla ya kuanza msimu kati ya mabingwa hao wa Bundesliga na Champions League na Barcelona katika uwanja wa Allianz Arena mnamo Julai 24 umeuza tikiti zote. Utakuwa mchuano utakaomleta kocha mpya wa Bayern Pep Guardiola na waajiri wake wa zamani ikiwa ni mwaka mmoja tu baada ya Mhispania huyo kuwachana na mabingwa hao wa Uhispania. Guardiola ambaye anajiunga na Bayern atafanya mazoezi yake ya kwanza mjini Munich Juni 26.
The Happy One
Jose Mourinho aliyeonekana uwa mtulivu hii leo amejipa jina jingine la “Happy One“ wakati akianza safari yake kama kocha wa Chelsea kwa mara ya pili, huku akitangaza mikakati yake ya kutaka kuiimarisha klabu ya Chelsea kwa mara nyingine katika Ligi Kuu ya Soka Enlgand.
Mreno huyo mwenye umri wa miaka 50 akizungumza kwa mara ya kwanza na waandishi wa habari katiak uwanja wa Stamford Bridge amesema yeye ni “mwenye furaha“. Amesema hata hivyo kwamba bado ana ari ile ile, bidii ile ile na maono yale yale aliyokuwa nayo wakati akianza taaluma yake kama kocha. Miaka tisa iliyopita Mourinho alijiita „Special One” wakati alipojiunga na Chelsea kwa mara ya kwanza.
Tennis
Katika tennis, Rafael Nadal ameweka historia jana, kwa kumpiku Mhispania mwenzake David Ferrer kwa seti za 6-3, 6-2, 6-3 na kunyanyua taji la French Open kwa mara ya nane. Ijapokuwa kulikuwa na tukio lililojaribu kuvuruga fainali hiyo ya jana wakati shabiki mmoja alipowasha fataki akipinga ndoa za jinsia moja nchini Ufaransa. Nadal, sasa ni mchezaji wa kwanza kunyakua mataji manane ya French Open katika kitengo cha mchezaji binafsi. Alikabidhiwa taji na bingwa mara sita wa Olimpiki, mwanariadha wa kasi Usain Bolt. Mhispania huyo ana mataji kumi na mawili ya Grand Slam, ikiwa ni upungufu wa matano kuliko aliyozoa Roger Federer.
Kwa upande wa wanawake, Serena Williams alimpiku bingwa mtetezi Maria Sharapova na kutwaa taji lake la 16 la Grand Slam. Alimpiku kwa seti za 6-4, 6-4 na kuendeleza msururu wa ushindi wake kufikia mechi 31. Serena anasema bado kuna mengi anayotarajia kufanya hata ingawa ana umri wa miaka 31.
Formula one
Na katika mbio za magari ya Formula One, ushindi wa Sebastian Vettel mbele ya Fernando Alonso katika kivumbo cha canadian Gnardn Prix unaonekana kuwa dalili za karibuni kwamba madereva hao wawili wanatarajiwa kuwa na vita vikali vya kuwania taji la Ulimwengu.
Vettel wa kampuni ya Red Bull aliongoza kutoka mwanzo hadi mwisho na kushinda kwa mara ya kwanza katika mkondo wa Gilles Villeneuve wakati Alonso akionyesha umahiri wa gari lake la Ferrari na kusonga kutoka nafasi ya sita hadi ya pili. Na wakati bingwa mara tatu wa Ulimwengu Vettel akiongeza pointi zake hadi 132 baada ya ushindi wake wa tatu msimu huu, Alonso alisonga katika nafasi ya pili na pointi 96, mbele ya dereva wa Lotus Kimi Raikkonen ambaye alimaliza katika nafasi ya nane na sasa ana pointi 88. Lewis Hamilton wa timu ya Mercedes alimaliza katika nafasi ya tatu katika mkondo wa jana na ana jumla ya pointi 77.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman