1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rouhani apongeza makubaliano ya nyuklia

17 Januari 2016

Rais Hassan Rouhani amesema Jumapili (17.01.2016) wale waliokuwa na mashaka ambao walionya makubaliano ya nyuklia na mataifa yenye nguvu hayatokuwa na manufaa kwa Iran "wote wamethibitishiwa kuwa walikuwa sio sahihi.

https://p.dw.com/p/1Hf30
Rais Hassan Rouhani katika mkutano na waandishi wa habari Tehran. (Jumapili 17.01.2016)
Rais Hassan Rouhani katika mkutano na waandishi wa habari Tehran. (Jumapili 17.01.2016)Picha: Getty Images/AFP/A. Kenare

Rouhani amewaambia waandishi wa habari mjini Tehran kwamba "masaa machache tu " baada ya kuanza kutekelezwa kwa makubaliano hayo ya nyuklia na kuondolewa kwa vikwazo "njia 1,000 za mikopo zimefunguliwa na benki mbali mbali."

Amesisitiza kwamba makubaliano hayo sasa yatarahisisha kampuni za Iran kufanya kazi baada ya kutengwa kwa miaka mingi katika mfumo wa fedha wa kimataifa.

Rais huyo amesema "leo tuko katika hali ambapo kwayo tunaweza kuwa na mawasiliano ya kisiasa,kiuchumi na kisheria na dunia kwa maslahi ya taifa."Ameongeza kusema "tunaamini umoja wetu wa kitaifa.Tunaamini mafanikio yetu ya taifa."

Aliuchezea kamari wadhifa

Matamshi yake hayo yalikuwa ni jibu kwa wale waliokuwa na mashaka waliosema kwamba mafanikio hayo ya kidiplomasia ya makubaliano hayo ya nyuklia hayawezi kutafsiriwa kwa vitendo vya faida ya kiuchumi kwa uchumi wa nchi hiyo.

Rais Hassan Rouhani wa Iran.
Rais Hassan Rouhani wa Iran.Picha: Reuters/J. Samad

Rohani aliuchezea kamari wadhifa wake wa urais kwa mazungumzo hayo ya nyuklia kwa kuimarisha juhudi za kidiplomasia na zenye kuhusisha Uingereza,China, Urusi,Ufaransa, Marekani na Ujerumani baada ya kuingia madarakani hapo mwezi wa Augusti mwaka 2013.

Ni wiki iliopita tu amesema wananchi wa Iran wanapaswa kusubiri kwa hamu "mwaka wa neema" baada ya nchi hiyo kuondolewa vikwazo.

Saudi Arabia yakosolewa

Rouhani pia amekosowa shutuma za Saudi Arabia kwa makubaliano hayo ya nyuklia kwa kumtaja afisa mmoja bila ya kulintangaza jina lake ambaye alisema kuondolewa kwa vikwazo ni hatua mbaya.

Waziri wa Mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif akishangiliwa bungeni kwa kufanikisha makubaliano ya nyuklia.
Waziri wa Mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif akishangiliwa bungeni kwa kufanikisha makubaliano ya nyuklia.Picha: Getty Images/AFP/A. Kenare

Akizungumzia hilo amesema "siku ya utekelezaji wa makubaliano hayo tumemuona afisa mmoja wa Saudia akielezea masikitiko yake kwamba matatizo ya kiuchumi ya Iran yamepatiwa ufumbuzi."

Amesema jirani hatakiwi kamwe kufanya hivyo.Muislamu hawezi kufanya hayo.Muislamu hatakiwi katu kukasirika kwa kufarajika kwa Muislamu mwenzake. Waislamu wote ni ndugu."

Hali ya mvutano

Kufuatia hatua ya Saudi Arabia nchi ya ufalme wa Kisunni kutekeleza adhabu ya kifo kwa sheikh wa Kishia Nimr al Nimr hapo Januari pili ubalozi wa Saudi Arabia mjini Tehran ulivamiwa kitendo ambacho kililaaniwa na Rais Rouhani.

Wakati ubalozi wa Saudi Arabia ulipovamiwa Tehran.
Wakati ubalozi wa Saudi Arabia ulipovamiwa Tehran.Picha: picture alliance/dpa/E. Noroozi

Siku moja kufuatia tukio hilo Saudi Arabia ilivunja uhusiano wake wa kibalozi na Iran.Rohani amesema mlango bado uko wazi kwa diplomasia lakini hauwezi kubakia wazi milele.

Amesema kile wanachotaka ni kutatua mizozo ya kanda hiyo kwa kutumia busara lakini wakati huo huo wananchi wao,serikali yao haitokubali hatua zisizo za kidiplomasia na zisizofaa.

Utekelezaji wa makuabaliano hayo ya nyuklia ya kihistoria kati ya Iran na mataifa yenye nguvu yanatarajiwa kufunguwa uhalisia mpya wa kiuchumi nchini Iran.

Zaidi ya dola bilioni 30 za mali za Iran zilizozuiliwa nchi za nje zitaachiliwa mara moja kwa serikali ya Iran.Jumla ya mali za Iran zilizozuiliwa nchi za nje ni dola bilioni 100.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/AP

Mhariri : Caro Robi