Rushwa, usalama kujadiliwa na viongozi wa Afrika
29 Juni 2018Zaidi ya wakuu wa matiafa 40 wanatarajiwa kuwasili katika mkutano huo wa mjini Nouakchott, ambao vilevile unatahudhuriwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, ambaye anatazamiwa kutoa msukumo katika jitihada za kiusalama katika ukanda wa Sahel. Rais wa Rwanda Paul Kagame, ambaye kwa hivi sasa ndiye anayeshikilia uenyekiti wa mataifa 55 yalio katika Umoja wa Afrika anatarajiwa kutoa wito wa kuhamasisha biashara huria.
Hadi wakati huu, kiwango cha biashara baina ya mataifa yenyewe ya Afrika asilimia 16 tu, kikiwa ni kiwango kidogo zaidi ukikilinganisha na maeneo ya kikanda kama ya Amerika ya Kusini, Asia, Amerika ya Kaskazini na Ulaya.
Hatua ya ukombozi wa kiuchumi Afrika
Mapema Machi mwaka huu matiafa 44 ya umoja huo yalisaini makubaliano yenye kuunda eneo kubwa kabisa la kibiashara duniani, yaitwayo CFTA. Mkataba huo ni matokeo ya mazungumzo ya miaka miwili, na unatajwa kuwa hatua muhimu kuelekea ufanikishaji mpana wa muingiliano barani humo.
Kama mataifa yote 55 wanachama yatatia saini, basi italifanya bara hilo kutengeneza pato lake la ndani dola trilioni 2.5 na kulifikia soko la watu bilioni 1.2. Lakini mataifa mawili yenye kuongoza kwa uchumi barani Afrika, Afrika Kusini na Nigeria, yanaonekana kutoukubali mpango wa CFTA. Hata hivyo, Rais Mohammad Buhari wa Nigeria anatarajiwa kuhudhuria mkutano huo wa Jumapili.
Lengo la kutunisha mfuko wa amani
Rais Kagame vilevile anatarajiwa kushinikiza mapendekezo yaliyodumu kwa takribani miaka miwili, yenye lengo la kutunisha mfuko wa mataifa ya Afrika wenye lengo la kupunguza hali ya utegemezi wa matiafa wahisani kwa mataifa hayo, hatua ambayo imeibua ukosoaji unaosema kuwa Umoja huo unaongoza kwa kusema huku utekelezaji wake kivitendo ukiwa sifuri kabisa.
Lengo ni kuweka kodi ya asilimia 0.2 kwa baadhi ya bidhaa zinazotoka nje ya bara hilo ili kutunisha fuko hilo lililopewa jina la "Mfuko wa Amani" kwa kuwezesha kusaidia jitihada za mipango ya ustawi wa amani na usalama. Katika kiasi cha dola milioni 769 cha bajeti ya Umoja wa Afrika, dola milioni 451 kinatoka kwa wafadhili, ambao pia wanashiriki kwa utekelezaji wa asilimia 97 ya programu mbalimbali za bara hilo.
Vita dhidi ya rushwa ni moja ya malengo rasmi ya mkutano huo wa kilele wa Umoja wa Afrika. Tatizo la rushwa litazingatiwa vyema katika kipindi hiki ambacho Afrika inajaribu kuondoa taswira yake mbaya ya kwamba ni moja kati ya eneo baya zaidi katika ufanyaji wa biashara. Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, yupo katika ratiba ya mkutano huo ya Jumatatu, lengo lake ni kutathimini hatua iliyopigwa na kikosi kinachopambana na ugaidi katika eneo la Sahel kinachoundwa na mataifa ya Burkina Faso, Chad, Mali, Mauritania na Niger.
Mwandishi: Sudi Mnette/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef