Safari ya treni kutoka Addis Ababa kwenda Djibouti.
Tangu mwanzoni mwa 2018, treni inayoendeshwa na wachina inasafirisha watu na mizigo kutoka Ethiopia kwenda mji wa bandari wa Djibouti. Mwandishi James Jeffrey alifanya safari kutoka Addis Ababa.
Mguso wa kichina
Nje kidogo ya mji wa Addis Ababa mtu anaweza kusamehewa kwa kudhani kasri la kichina limejengwa pasipofaa. Kituo hicho cha treni kinaonesha mwanzo wa reli mpya ya kutoka Addis Ababa kwenda mji wa Djibouti inayobeba abiria tangu Januari 2018. Ni mradi wa pamoja wa kampuni ya reli ya Ethiopia na Djibouti (EDR) na China ambayo ilijenga na kwa sehemu kubwa kugharamia mradi huo wa dola bilioni 4.
Kanuni na taratibu
Wasimamizi wa eneo la kupandia waliovalia vizibao vyekundu na kofia wanawakaribisha abiria kwenye treni ya saa mbili asubuhi kwenda Djibouti. Wachina ndiyo wanaendesha shughuli za reli hiyo kwa miaka sita ya mwanzo. Kondakta wa teni ni mchina kadhalika na wafanyakazi wa matengenezo katika karakana ya treni.
Mji unaachwa nyuma
Punde baada ya mji wa Addis Ababa ni mashamba ya kijani, vijumba vya kijijini na wanyama wanaotembea pembezoni mwa reli. ´´Kiwango cha wanyama pembezoni mwa njia hii ndiyo sababu kuu ya kupunguza mwendokasi wa treni´´ anasema Wang Hugue, meneja operesheni wa kichina. ´´mwanzo kulikuwa na matatizo kidogo na wakaazi.´´ Hivi sasa wakaazi hapa wanalipwa fidia kwa kila mnyama anayegongwa na treni.
Safari ya starehe
"Kabla, kusafiri kwa basi ilikuwa vigumu sana na ilifaa ubadili mabasi na kukesha. ilichukua karibu siku nzima na nusu kutoka Addis kwenda Djibouti," anasema Linda, mwalimu wa kiingereza kutoka Djibouti anarejea kutoka Addis Ababa. Safari ya treni ni saa 12 lakini walau ni ya kustarehe.
Kutia hina ili kupitisha muda
Huduma ya abiria bado inatolewa chini ya kiwango na abiria wana nafasi ya kutosha kwa shuguli kemkem ikiwemo kupaka hina. Lakini huduma ya abiria siyo kipaumbele cha treni hii. Treni nne za mizigo zinasafiri kila siku- mbili kutoka kila upande- kila moja ikibeba kontena 106 ya bidhaa ambazo mahitaji yake yanaongezeka na zimezalishwa katika uchumi wa Ethiopia uliovurugika.
Mahaba na cha zamani
Reli mpya kwa sehemu inapita sambamba na reli ya zamani iliyojengwa mwanzoni mwa karne ya 20."Ingekuwa hiyari yangu, ningepanda treni ile ya zamani" anasema Julius, raia wa Ethiopia anayekwenda Djibouti kumtembelea shangazi yake. "Wakati ule ulikuwa unaona miji treni iliposimama, unasikia lugha mbalimbali, tamaduni na watu wa maeneo hayo. Treni hii inakwenda moja kwa moja na kupita kila kitu."
Treni inapata uchangamfu
Baada ya kusimama katika mji wa Dire Dawa karibu nusu ya safari ya kilometa 728, mabehewa yamejaa abiria wanaozungumza mchanganyiko wa kiamhari, kisomali na kifaransa (Djibouti ilikuwa koloni la Ufaransa), huku wakibadilishana mifuko ya vyakula. Hata muziki uliokuwa ukichezwa ndani ya treni ni wa kuchangamka wakati safari ikiendelea.
Muda wa kutafuna mirungi
"Ilibidi kubadilika kwa kweli" anasema msimamizi wa Treni Hugue. Abiria walikuwa wakibeba mirungi, mmea unaotafunwa sehemu kubwa ya pembe ya Afrika, ambao umepigwa marufuku na unazingatiwa kuwa dawa ya kulevya nchini China. "Mwanzoni hatukuruhusu, lakini Kampuni ya EDR ikasema ni sehemu ya utamaduni, na tukakubali hatuwezi kuharibu tamaduni na inafaa kuheshimiana kila mmoja"
Mwelekeo sahihi
Ikiwa zimesalia kilometa 200, jua linaanza kuzama katikati ya jangwa na mabehewa yanaanza kupunguza kelele. Wachambuzi wa siasa wanaamini kuwa njia mpya ya reli na uhuru wa kusafiri na shughuli za kiuchumi zinazoambatana nazo, ni ushahidi wa kuimarika kwa amani na ushirkiano katika pembe ya Afrika.