1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Safari ya Uganda ya medali ya Olimpiki

11 Septemba 2012

Baada ya miaka 40 ya kusubiri, bendera ya Uganda ilipeperushwa tena katika jiji la London, nchini Uingereza, kufuatia ushindi murua wa mwanariadha wake, Stephen Kiprotich katika mashindano ya mbio za masafa marefu.

https://p.dw.com/p/166gD
Uganda's Stephen Kiprotich waves his national flag as he crosses the finish line to win the athletics event men's marathon during the London 2012 Olympic Games on August 12, 2012 in London. AFP PHOTO / DANIEL GARCIA (Photo credit should read DANIEL GARCIA/AFP/GettyImages)
Olympia 2012 Marathon Stephen KiprotichPicha: Getty Images

Stephen Kiprotich asingechagua wakati mzuri zaidi kushinda medali ya dhahabu katika mashindano ya Olimpiki ya mjini London. Kwa ushindi wa medali hiyo, wimbo wa taifa wa Uganda ulijumuishwa katika ratiba ya kufunga mashindano hayo, jioni ya Jumapili tarehe 12 Agosti mwaka 2012. Zawadi kwa kushinda siku hiyo, ilikuwa kukabidhiwa medali yake ya dhahabu na rais wa kamati ya Olimpiki ya dunia, Jacque Rogge na mkuu wa shirikisho la riadha duniani, Lamine Diack. Kiprotich alifurahia dhahabu yake mbele ya hadhira ya watu zaidi ya bilioni moja, ambao hawakuwa na tukio lingine la kushuhudia ukiacha hilo la mwisho kabisaa la kukabidhiwa kwake medali ya dhahabu. Lakini medali hiyo ina maana gani kwa Uganda na kwake binafsi?

"Ina maana kubwa, maana kubwa sana. tangu mwaka 1972 hatujawahi kushinda medali ya dhahabu, nina furaha kubwa kushindwa medali hii kwanza kwa ajili yangu, kwa ajili ya nchi yangu, kwa ajili ya familia yangu na kwa ajili ya kila raia wa Uganda na dunia nzima. Sasa naweza kufa nikiwa bingwa na siyo kama mtu asiye na manufaa kwa nchi yangu. Sasa hivi mimi ni mtu muhimu katika nchi yangu," alisema Kiprotich.

Lilikuwa ni jambo ambalo halikufikirika hapo awali, kuwa Kiprotich angeweza kufurukuta mbele ya wakenya, mshindi wa mbio za London, Wilson Kipsang na bingwa wa dunia, Abel Kirui, ambao waliongoza mbio hizo kabla ya mganda huyo kuwachomoka na kushinda katika muda wa saa mbili dakika nane na sekunde moja huku Kirui na Kipsanga wakishika nafasi ya pili na ya tatu kwa muda wa saa mbili dakika nane na sekunde 27 na saa mbili dakika tisa na sekunde 37.

Magazeti nchini Uganda, ambayo hapo awali yalikuwa hayampi umuhimu mkubwa Kiprotich hasa baada ya kushindwa kwa tegemeo la wengi, Moses Kipsiro yalichapisha kurasa za mbele zikiwa na sura ya Kiprotich yakitoa sifa kwa shujaa huyo, kijana wa umri wa miaka 23 aliyewashindwa wakimbiaji 105 kutoka mataifa 68. Gazeti huru la kila siku la Daily Monitor lilitoka na kichwa kisemacho: Uokovu wakitaifa. Gazeti la serikali la New Vision halikuwa na kitu kingine kwenye ukurasa wake wa mbele zaidi ya jina la Kiprotich na picha yake ya ushindi wa mbio hizo za kilomita 42.

Ni furaha iliyoje!!!

"Nilifurahi sana, unajua nilikuwa naendesha gari nikiende kushiriki duwa kwa baba'ngu. Lakini nilikuwa najua kuwa Kiprotich alikuwa katika kundi la watu watatu waliokuwa wanaongoza, wakenya wawili na yeye akiwa wa tatu. Nikasema hata tusipopata medali ya dhahabu, angalau tungepata hata ya fedha au shaba. Ghafla nikasikia mripuko wa vifijo na vigelegele nikajua tumeshinda. lakini furaha yangu ilizidi na nikatokwa na machozi pale wimbo wetu wa taifa ulipopigwa wa mwisho kabisaa," alisema Sarah Sengooba ambaye alikuwa akifuatilia mashindano kwa karibu.

Uganda pia ilishinda dhahabu yake ya mwisho barani Ulaya, katika mashindano yaliyofanyika jijini Munich nchini Ujerumani, ambapo John Akii Bua ambaye alikuwa afisa wa jeshi la Polisi, alishinda medali ya dhahabu katika mbio za kuruka vihunzi na kuwa mwafrika wa kwanza kushinda mbio hizo katika muda mfupu zaidi. Huo ulikuwa mwaka 1972 na rais wa Uganda wakati huo Jemedari wa jeshi Iddi Amin Dada alimzawadia nyumba, gari mpya na kisha kuupa uwanja mmoja wa michezo jina lake. Lakini sasa uwanja huo umeshagawiwa na serikali na jambo hili linamsikitisha Sunday Bashaija, mwandishi wa michezo na ambaye pia aliwahi kuwa mwanariadha.

"Wanauza viwanja vyetu vya michezo. Karibu nchi nzima havipo tena na hakuna hata sehemu ya kufanyia mazoezi. Uwanja uliojengwa kama kumbukumbu ya John Akii Bua umegawiwa miaka michache iliyopita. Najisikia vibaya," anasema Bashaija.

Harambee ya kumtuza Kiprotich

Kampuni ya Vision Group iliendesha harambee na kuafanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi za Uganda milioni 300 ambazo zilikabidhiwa kwa Kiprotich kama zawadi kwa shujaa huyo mpya aliyewafuta machozi waganda na kuwapa matumaini mapya na nchi yao. Rais wa Uganda, Yowei Museveni, naye alimpa zawada Kiprotich kitita cha dola 80,000 na kuahidi kuwajengea wazazi wake wanaoishi katika nyumba ya nyasi na udongo, nyumba ya kisasa. Museveni pia alimualika Kiprotich na familia yake katika Ikulu ya rais mjini Entebbe ambako alimkabidhi hundi yake.

Lakini wakati hali ikiwa ni ya furaha miongoni mwa raia wengi wa Uganda, waziri anayehusika na masuala ya michezo alikuwa na wakati mgumu akikabiliwa na maswali magumu kutoka kwa wabunge wa nchi hiyo waliotaka kujua kwa nini serikali haiipi kipaumbele sekta ya michezo na badala yake inasubiri wanamichezo wafanikiwe kwa juhudi zao wenyewe na kisha serikali kudai mafanikio hayo. Haya na majibizano kati ya wajumbe wa kamati ya huduma za jamii ya Bunge la Uganda na waziri wa michezo wa nchi hiyo, Charles Bakkabulindi.

Madai ya wizi wa vifaa vya wanariadha pia yaliibuliwa katika kikao hicho ambapo madai ya kuibwa kwa vifaa vya wanariadha wa Uganda mjini London yalitolewa, huku ikidaiwa zaidi kuwa vifaa hivyo viliibiwa na maafisa waliyoambatana na timu ya riadha ya Uganda kwenda jijini London. Hii ni baada ya mwanariadha wa kike Dorcas Inzikuru kupotelewa na vifaa vyake na kulazimika kutafuta vingine, jambo ambalo liliathiri utendaji wake.

Ushindi wachochea hamasa ya kuwekeza katika michezo

Ushindi wa Kiprotich uliibua mjadala mkubwa kuhusiana na uwezo wa Uganda katika sekta ya michezo. Mwenyewe anasisitiza kuwa wapo vijana wengi nchini humo wenye vipaji vya michezo lakini kikwazo kikubwa ni miundombinu na vifaa vya kuwawezesha kutumia vipaji vyao.

Kutokana na utamu wa ushindi huu serikali ya Uganda sasa imetangaza kuwekeza katika kukuza vipaji vya michezo. Imetangaza shule 32 za sekondari ambazo zitageuzwa kuwa vituo vya kukuza vipaji vya michezo na wizara ya michezo imesema inahitaji shilingi za Uganda bilioni sita ili kufanikisha azma hiyo.

Raia wa Uganda huwa wana mashaka na ahadi zinazotolewa na serikali yao kutokana na ukweli kuwa nyingi hazitekelezeki. Lakini kisicho na mashaka ni kwamba wote walipata sababu ya kujivunia utaifa wao wakati ambapo Uganda inajiandaa kusherehekea miaka 50 ya Uhuru wake kutoka utawala wa Uingereza. Ndiyo maana haishangazi hata Kiprotich aliipatia nchi yake nafasi ya 50 katika mashindano ya Olimpiki.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Charo Josephati Nyiro.