Salva Kiir na Riek Machar wakubaliana kudumisha amani
27 Juni 2018Viongozi mahasimu wa kisiasa nchini Sudan Kusini rais Salva Kiir na kiongozi wa waasi, Riek Machar wametia saini makubaliano ya amani mjini Khartoum, ambapo chini ya makubaliano hayo, wameridhia kutekeleza katika kipindi cha saa 72 hatua ya kudumu ya kusitisha mapigano.
Hatua hiyo imeibua matumaini kwamba mkataba huo utahitimisha vita vya muda mrefu vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo. Waziri wa mambo ya nje wa Sudan Al-Dierdiry Ahmed ametangaza mwafaka huo baada ya kufanyika mazungumzo katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum.
Amesema pande zote zimekubaliana usitishwaji wa kudumu wa mapigano utakaoanza ndani ya masaa 72. Kiir na Machar wamesaini waraka mbele ya rais wa Sudan, Omar Al Bashir.
Baada ya kutiliana saini, Kiir alisema hii ni siku ambayo raia wengi wa Sudan Kusini waliitarajia. Machar alisema, usitishwaji huu wa mapigano ni lazima uwe mwelekeo wa kumaliza mapigano. Juhudi mpya za amani za Sudan Kusini zilianzishwa na viongozi wa Afrika Mashariki.
(Mtangazaji wa habari Caro Robi amemhoji balozi wa Sudan Kusini nchini Ethiopia James Pitia Morgan ambaye kwanza anafafanua kuhusu makubaliano hayo. Yasikilize mahojiano hayo hapa)