1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saratani: Janga la kitaifa nchini Kenya

31 Oktoba 2018

Mamia kwa maelfu ya wakaazi wa mkoa wa Pwani nchini Kenya walikusanyika mjini Kilifi mkoani humo kwa zoezi la kufanyiwa uchunguzi na matibabu ya bila malipo kwa watu wanaougua Saratani.

https://p.dw.com/p/37S0W
Labor Analyse Blutuntersuchung Pipette Objektträger
Upungufu wa vifaa, bado tatizo kubwa linalosababisha changamotoPicha: picture-alliance/dpa/Media for Medical

Maradhi hayo ya saratani sasa yanatajwa kuwa janga la kitaifa baada ya janga la maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, huku wito ukitolewa kwa mataifa ya ulimwengu na wafadhili kuelekeza juhudi zao katika kupambana na kuongezeka kwa visa vya Saratani. 

Zoezi la leo linahitimisha matembezi yaliyochukua muda wa mwezi mzima kwa kina mama Watatu ambao wametembea kutoka Mji wa Kisumu ulio mkabala na Ziwa Victoria Magharibi mwa Kenya hadi Mkoani Pwani, yapata umbali wa kilomita 850, lengo kubwa likiwa kuihamasisha jamii kuhusu janga la Maradhi haya Saratani nchini Kenya.

Kwa hakika ni Idadi kubwa sana iliyojitokeza leo kufanyiwa uchunguzi dhidi ya maradhi haya ya Saratani na kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na idara ya Afya nchini Kenya, Zaidi ya visa elfu 39 hurekodiwa kila mwaka na watu 27 alfu kati yao hufariki kutokana na Saratani. Hii ni kiwango cha asilimia 60 ya watu wanapugua Saratani.

Saratani ya Mlango wa kizazi ndiyo husababisha vifo vingi Zaidi nchini Kenya, ikifuatia na ile ya Koo na Matiti akijitika katika kiwango cha asilimia 34 ya visa hivyo.

Indien Forschungsstudie Gebärmutterhalskrebs
Picha: A. Budukh

Tatizo kubwa linalotajwa kuchangia kuongezeka kwa visa vya Ugonjwa wa Saratani nchini Kenya, ni ukosefu wa vifaa katika Hospitali nyingi tu kuwa fanyia uchunguzi wa mapema watu wanaugua maradhi hayo. Tatizo jingine hasa kwa Kinamama wanaougua Saratani ya Mlango wa Kizazi ni ukosefu wa ufahamu kuhusu mpango wa Uzazi.

Akizungumza wakati wa shughuli hiyo ya uchunguzi na matibabu ya bila Malipo, Mke wa Gavana wa Kaunti ya Kisumu Bi Dorothy Nyon'go, alisema kuwa ipo haja ya serikali ya Kenya sasa kutangaza Saratani kuwa janga la kitaifa na kuelekeza rasilimali Zaidi katika kuwahamasisha raia wake athari za Ugonjwa huu.

Akiwa mfadhili mkuu wa Matembezi haya Dorothy Nyong'o ambaye pia ni Mamake Muigizaji maarufu Ulimwenguni Lupita Nyomg'o , Zaidi alisema kuwa mabadiliko ya maisha hususana aina mbali mbali ya vyakula, vimechangia pakubwa kuongezeka kwa visa vya saratani nchini Kenya huku akisikitika kwamba ni asilimia 14 pekee ya Kinamama ambao hufika hospitalini kufanyiwa uchunguzi dhidi ya Saratani kila mwaka.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Waziri wa Afya Jimbo la Kilifi Dkt Anisa Omar akisema kuwa kutokana na hali ngumu ya Maisha, jimbo la Kilifi pekee hurekodi jumla ya Visa 15 vya Ugonjwa wa Saratani kila mwezi.

Mwandishi: Eric Ponda

Mhariri:Yusuf Saumu