Schalke 04 yabumburushwa na Maribor
1 Oktoba 2014Kwa kile ambacho wengi wamekiita kuwa ni timu dhaifu zaidi katika Kundi G la Champions League, klabu ya Maribor kutoka Slovenia inadhihirisha kuwa timu imara ambayo inaweza kupata matokeo mazuri. Vijana hao wa Kocha Ante Simundza wanaweza kuwa na furaha kutokana na pointi waliyopata baada ya kutoka sare ya goli moja kwa moja na Schalke iliyopigiwa upatu na wengi kupata ushindi wa urahisi.
Maribor ilionekana kuwa imara katika dakika za mwanzo za mchezo, na kuwabumburusha Schalke katika dakika ya 37, wakati Mitja Viler ambaye alikuwa peke yake katika upande wa kushoto wa uwanja, alipopata mpira kutokana na krosi ndefu na akamwandalia pasi safi Damjan Bohar, ambaye hakuchelewa kusukuma kombora safi sana lililomshinda maarifa kipa wa Schalke Ralf Färmann.
Uongozi wa wageni ulidumu hadi dakika ya 56 wakati Klaas-Jan Huntelaar alipombwaga beki wa Maribor Aleksander Rajcevic na akaweka mpora ndani ya nyafu huku kipa Jasmin Handanovic asiwe na la kufanya.
Kuanzia hapo Schalke waliumaliza mchezo hukuwa wakiutawala mchezo kuliko namna walivouanza, lakini matumaini ya Maribor yaliongezeka na kuwawezesha kuondoka Ujerumani na point moja muhimu.
Maribor na Schalke wana points mbili kila mmoja katika kundi lao baada ya kutoka sare ya goli moja kwa moja katika mechi mbili. Chelsea, ambao walitoka sare na Schalke katika mechi ya kwanza waliipiku Sporting LISBON bao moja kwa sifuri katika mchuano wa pili na sasa wanaongoza kundi G wakiwa na points nne. Sporting ni wa mwisho na point moja pekee. Schalke watashuka dimbani na Sporting LISBON katika mechi nyingine ya nyumbani mnamo Oktoba 21, wakati Chelsea ikiwaalika Maribor siku hiyo hiyo.
Mwandishi: Bruce Amani/DW
Mhariri: Mohammed Khelef