Seleka Wako Tayari Kuzungumza
2 Januari 2013Kipindi cha kuweka chini silaha kinaweza kuwa kifupi kwa rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Francois Bozizé, ambaye waasi wa Seleka wanamtaka ajiuzulu.
"Nimewataka wanajeshi wetu wasisonge mbele kutoka mahala waliko hivi sasa kwa sababu tunataka kushiriki katika mazungumzo ya Libreville ili kusaka ufumbuzi wa kisiasa," amesema msemaji wa waasi, Eric Massi kwa njia ya simu kutoka Paris, Ufaransa.
Ameongeza kusema "anaendelea kushauriana na washirika wao ili kuandaa mapendekezo ya kumaliza mvutano yatakayofanikisha kama anavyosema "kuundwa kipindi cha mpito bila ya kushirikishwa rais Bozizé."
Jumapili iliyopita rais huyo alisema yuko tayari kugawama madaraka na waasi wa Seleka na kuridhia kushiriki katika meza ya mazungumzo ya amani bila ya masharti.
Kwa mujibu wa duru za kidiplomasia, mazungumzo ya Libreville huenda yakaanza Januari 10 ijayo.
Wakaazi wa Bangui Washusha pumzi
Pendekezo la Seleka limepokelewa vyema mjini Bangui, ambako tangu siku kadhaa zilizopita, wakaazi wake wamekuwa wakikusanya mahitaji yao ya kila siku ili kukabiliana na kitisho cha mashambulio.
"Wanasema hawataki kuushambulia mji mkuu Bangui, na hizo ni habari za kutia moyo kwetu." Bora kwa kila upande ikiwa wataketi katika meza ya mazungumzo," amesema mkaazi mmoja akionyesha jinsi anavyofurahia uamuzi wa Seleka.
Jumuiya ya ushirikiano wa kiuchumi ya nchi za Afrika kati, inayozileta pamoja Chad, Jamhuri ya Kongo, Gabon na Cameroon, imetuma kikosi cha wanajeshi elfu tano katika Jamhuri ya Afrika kati, nchi mojawapo masikini kabisa ya dunia licha ya utajiri mkubwa wa madini ya urani, dhahabu na almasi. Idadi hiyo huenda ikaongezeka na kufikia wanajeshi 760 hadi mwishoni mwa wiki hii.
Vikosi vya Afrika Kati Vyawaonya Waasi
Katika wakati ambapo waasi wa Seleka wametangaza kutosonga mbele kuelekea mji mkuu Bangui, hali inasemekana ni tete na visa vya umwagaji damu kuripotiwa tangu vijijini mpaka katika mji mkuu Bangui.
Mkuu wa kikosi hicho, jenerali Jean Felix Akaga, amewaonya waasi dhidi ya hatua yoyote ya kuuteka mji wa Damara ulioko umbali wa kilomita 75 karibu na Bangui, akisema tukio hilo litaangaliwa kuwa ni sawa na tangazo la vita.
Wakati huo huo, watu wanne wameuwawa, wawili kati yao wakiwa ni waasi wa Seleka, kufuatia mapigano kati yao na wakaazi wa kijiji cha Ngakobo, karibu na mji wa Bambari, katika eneo la kati la Jamhuri ya Afrika kati.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters
Mhariri:Josephat Charo