Sera ya Uchumi ya ANC ya Zuma yawapa wasi wasi wawekezaji
21 Oktoba 2008Chama cha tawala Afrika kusini African National Congress-ANC na washirika wake chama cha kikoministi na Shirikisho la vyama vya wafanyakazi,walizindua hivi karibuni waraka wa kiuchumi ambao umeitwa kuwa ni wa kuzingatia hali za walala hoi , na kutoa kipa umbele katika vita dhidi ya dhidi ya umasikini na ukosefu wa ajira, kuhoji sera ya kudhibiti mfumko wa bei na kutaja juu ya dola kujiingiza zaidi katika masuala mbali mbali.Lakini tayari wachambuzi wanasema hayo ni shida kutekelezwa kwa sababu mbali mbali ,ikiwa ni pamoja na athari za msukosuko wa fedha duniani.
Kiongozi wa ANC Jacob Zuma ameahidi kutozipa mgongo sera za Afrika kusini wakati huu za kuiunga mkono sera ya biashara ikiwa atashinda uchaguzi mwaka ujao, lakini wawekezaji wana wasi wasi kwamba atasalimu amri mbele ya washirika wake wa siasa za mrengo wa shoto.
Baadhi ya magazeti ya Afrika kusini yanauelezea mpango wa kiuchumi wa ushirika makundi hayo matatu, ANC, chama cha kikoministi na Shirikisho la vyama vya wafanyakazi kama ushahidi kwamba hali inaweza ikabadilika.
Lakini pamoja na hayo wachambuzi wanaashiria kwamba, kutokana na msukosuko katika masoko ya kimataifa, gharama kubwa za kukopa kwa sababu ya msukosuko wa fedha duniani na pia uhaba mkubwa wa wafanyakazi wenye ujuzi-yote haya huenda yakakiwia vigumu chama cha ANC, kutekeleza mipango yake ya sera za bawa la shoto na kuwa mabadiliko makubwa ya sera nchini humo.
Tayari kiwingu cha kutofahamika hali itakuaje baadae, kimeshazusha hofu miongoni mwa wawekezaji na katika kuzituliza, Rais Kgalema Motlanthe alishika hatamu hadi uchaguzi mkuu ujao,baada ya Thabo Mbeki kulazimishwa kuachia madaraka alimteuwa tena waziri wa fedha anayesifika ndani na nje ya nchi hiyo Trevor Manuel kuendelea na wadhifa huo.
Kinyume na Manuel anayependelea na kuunga mkono sera za soko huria, ANC chini ya Zuma na washirika wake wametoa wito wa mpango wa kugawa utajiri na sera imara zaidi ya viwanda, ikiwa na maana kuundwa makampuni yatakayosimamiwa na serikali.
Lakini Moeletsi Mbeki makamu mwenyekiti wa taasisi ya masuala ya kimataifa ya Afrika kusini anasema"wawekezaji hawapaswi kuwa na hofu yoyote, matamshi yote haya ya sera kali za mrengo wa shoto ni maneno matupu."
Ama jambo jengine linalotajwa na wadadisi kuwa huenda likasababisha hayo yasifanikiwe ni uwezekano wa kuundwa chama kipya na watakaojiengua katika ANC. Wengi wao huenda wakawa ni wale wafuasi wa Mbeki na wenye siasa za wastani.
Hilo linaweza kutoa upinzani na changamoto kubwa kwa ANC, kwa mara ya kwanza tangu kumalizika utawala wa wazungu wachache 1994. Wakati huo litakua ni chaguo la mambo mawili kwa wenye siasa za wastani watakaoamua kubakia ANC, kufanya juhudi za kudhibiti hatamu chamani au nao kukihama na kukipa msukosuko zaidi na kukidoofisha.