1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Congo yadaiwa kutekeleza mauaji kwa raia wake

Mjahida 18 Novemba 2014

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch limeishutumu polisi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa mauaji ya watu 51, katika oparesheni ya kuwakamata wahalifu nchini humo.

https://p.dw.com/p/1Dp5x
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph KabilaPicha: Reuters

Ripoti hiyo ilioandikwa kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa na watu walioshuhudia visa hivyo, ni uchunguzi wa pili kufanywa juu ya oparesheni hiyo ilioanzishwa mwezi Novemba, ya kuwasaka wahalifu nchini humo, inayojulikana kama Likofi kwa lugha ya kilingala.

Serikali ya Kinshasa hata hivyo haikuweza kupatikana haraka kutoa maoni juu ya ripoti hiyo, lakini waziri wa ndani Richard Muyej awali alitupilia mbali madai kama hayo yaliokuwa katika ripoti ya Umoja wa Mataifa na badala yake akawashutumu waliyoiandika ripoti hiyo kwa kujaribu kuidhoofisha serikali ya Congo.

Shirika la Human Rights Watch limedai polisi waliohusika katika oparesheni hiyo kwa waliwauwa vijana waliokuwa hawana silaha waliokuwa nyumbani kwao na familia zao. Vijana wengine waliuliwa sokoni na hata katika maeneo ya wazi hii ikiwa ni nia moja ya kuwatisha wakaazi wa eneo hilo.

Nembo ya shirika la kukutea haki za binaadamu HRW
Nembo ya shirika la kukutea haki za binaadamu HRW

Kwa upande wake mamake kijana mmoja aliyeuwawa kwa kupigwa risasi amesema anakumbuka namna polisi waliofunika nyuso zao walivyowaambia watu waliokuwa karibu wakati wa mauaji ya mtoto wake kwamba njooni muone tumemuua 'kuluna' yani mhalifu aliyewafanya mtaabike.

Waliouwawa wanasemekana kutohusika kwa aina yoyote na uhalifu

Shirika hilo la kutetea haki za binaadamu limesema baadhi ya waathiriwa hawakuhusika na uhalifu wa aina yoyote na wala hawakutishia usalama au kufanya lolote ambalo lingewafanya wauwawe.

Human Rights Watch imesema huenda kukawa na mauaji zaidi kuliko yale walioyoyaripoti. Naye polisi aliyezungumza na shirika hilo alisema huenda ikawa zaidi ya watu 100 ndio waliouwawa.

Kwa upande mwengine ofisi ya shirika la kutetea haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa (UNJHRO) ilio nchini Congo, nayo pia iliandika ripoti yake mwezi wa Oktoba iliyowashutumu polisi wa nchi hiyo kuwauwa watu tisa katika oparesheni iliomalizika mwezi wa February.

Ramani ya Congo
Ramani ya Congo

Muda mfupi baada ya ripoti hiyo serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikamfukuza nchini humo mkuu wa ofisi hiyo Scott Campbell hatua iliolikasirisha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililoripoti vitisho kwa wafanyakazi wa UNJHRO.

Kwa upande mwengine katika kutuliza ukosoaji wa kimataifa, Waziri wa ndani wa Congo Richard Muyej aliwakusanya mabalozi mjini Kinshasa na kuwaambia serikali iko tayari kufanya kazi na shiria la UNJHRO.

Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman