1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya DRC yagawa vyandarua dhidi ya mbu

Mitima Delachance, Bukavu,5 Septemba 2019

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeanza kampeni ya kupambana na ugonjwa wa Malaria katika eneo la Kivu Kusini kwa kugawa vyandarua kwa wananchi.

https://p.dw.com/p/3P3MB
Denguefieber in Pakistan
Picha: DW/A.Bacha

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imeanzisha ugavi wa vyandaruwa vya kujikinga dhidi ya mbu katika mkoa wa Kivu kusini, ili kuchangia katika kupambana na ugonjwa wa Malaria. Shughuli hizo zimeanzishwa wakati wakaazi wa mkoa huo wakiwa na maoni tofauti kuhusu matumizi ya vyandaruwa hivyo. 

Wakati wa uzinduzi wa kampeni ya ugavi wa vyandarua hivyo vyenye nguvu ya muda mrefu ya kuuwa mbu, gavana wa Kivu Kusini Theo Ngwabidje alisema vyandarua vinatolewa bila malipo yoyote.

Kwa mujibu wa wizara ya afya, watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na wanawake wajawazito, ndio wanaokabiliwa na kitisho zaidi cha kuugua Malaria. Hayo yamesemwa na daktari Claude Bahizire ambaye ni afisa anayehusika na mawasiliano kwenye idara ya afya Kkvu Kusini. Anabainisha kuwa tangu Januari hadi mwezi wa Juni mwaka huu, watu 500,000 tano wameugua malaria katika mkoa wa Kivu Kusini, na 308 wamefariki :

Mbu hufyonza damu na husababisha ugonjwa wa Malaria.
Mbu hufyonza damu na husababisha ugonjwa wa Malaria.Picha: picture alliance/dpa

"Ukichunguza takwimu, ni hasa zaidi watoto wachanga ndio wanaathirika kwa asilimia arobaini na saba, na wanawake wajawazito kwa asilimia ine nukta mbili. Na visa hivi ni vile vilivyoripotiwa katika vituo vya afya. Hapo bado vile visa vingine vingi visivyojulikana sababu ya kutopelekwa hospitalini. Ikiwa hali hii itaendelea, mwisho wa mwaka huu huenda visa vya Malaria vitafikia 2,000,000." Amesema daktari Claude Bahizire

Lakini maoni ya wakaazi yanazidi kutofautiana kuhusu matumizi ya vyandarua. Mkaazi mmoja kwa jina Christine amesema "Maeneo yaliyo athirika zaidi na ugonjwa wa Maleria ni hasa wilaya za Fizi na Kalehe upande wa Minova na Numbi si hapa" Naye Déchoc Bin Nyongolo ambaye ni mkaazi wa Kamanyola. Anahisi kwamba Juhudi za kupambana na Malaria katika mkoa huu zinakumbwa na changamoto chungu nzima, zikiwemo imani za kidini, imani potofu kuhusu ulinzi wa mazingira, na kadhalika.

Mnamo siku za hivi karibuni kunashuhudiwa ongezeko la visa vya ugonjwa wa Malaria katika mkoa wa Kivu Kusini. Wizara ya afya inaendelea kuhimiza wakaazi kuhusu ulinzi bora wa mazingira kwa kukausha maji yanayotuama na kusababisha kuzaliana kwa mbu.