1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir ashutumiwa kwa mapigano Juba

9 Septemba 2016

Jopo la wataalam wa Umoja wa Mataifa limekamilisha uchunguzi wake na kubaini kuwa mapigano makali yaliyoukumba mji mkuu wa Sudan Kusini Juba mwezi Julai mwaka huu yalitokana na maagizo ya ngazi za juu nchini humo.

https://p.dw.com/p/1JyrW
Rais wa Sudan Kusini , Salva Kiir
Rais wa Sudan Kusini, Salva KiirPicha: Getty Images/AFP/M. Sharma

Jopo la wataalam wa Umoja wa Mataifa limekamilisha uchunguzi wake na kubaini kuwa mapigano makali yaliyoukumba mji mkuu wa Sudan Kusini Juba mwezi Julai mwaka huu na kusababisha aliyekuwa Makamu wa Rais wa nchi hiyo Riek Machar kuondoka katika mji huo yalisababishwa na maagizo yaliyotolewa na ngazi za juu za jeshi la serikali ya nchi hiyo. Isaac Gamba anaarifu zaidi katika taarifa ifuatayo.

Taarifa hiyo ya siri ambayo pia imekaririwa hapo jana na shirika la habari la AFP inamnyooshea kidole Rais Salva Kiir na mkuu wa majeshi nchini humo Paul Malong kwa kuagiza kuanzisha upya mashambulizi yaliyoanza Julai 8, mwaka huu.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo mashambulizi hayo ambayo yalienda sambamba na matumizi ya Helikopta za kivita chapa MI-24 pamoja na mashambulizi ya vikosi vya ardhini yanaashiria kuwa yalitokana na maagizo kutoka ngazi za juu za utawala wa nchi hiyo chini ya mwongozo wa serikali.

Rais Salva Kiir alaumiwa kwa kuamuru mashambulizi mapya

Katika ripoti hiyo jopo hilo limemnukuu afisa mmoja wa serikali ya Sudan Kusini akisema kuwa Rais Salva Kiir pamoja na mkuu wa majeshi Paul Malong ndio pekee walio na mamlaka ya kuamuru helikopta kwenda vitani na kuwa mkuu huyo wa majeshi aliamuru hilo akijua fika kuwa Rais Salva Kiir alikuwa akifahamu kilichokuwa kinaendelea.

Kindersoldat Südsudan
Picha: picture-alliance/dpa/S.Bor

Zaidi ya watu 300 waliuawa katika mapigano hayo yaliyoanza tarehe 8-11, Julai mwaka huu huku maelfu ya raia nchini humo wakilazimika kuyahama makazi yao na kusababisha kusambaratika kwa serikali ya Umoja wa kitaifa iliyodumu kwa muda wa mwaka mmoja ambayo ilitokana na kusainiwa kwa mkataba wa amani na pande zote mbili zinazohasimiana nchini humo kwa lengo la kumaliza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.

Umoja wa Mataifa umeripoti juu ya kuwepo kwa udhalilishaji wa kingono dhidi ya wanawake na watoto uliofanywa zaidi na wanajeshi wenye asili la kabila la Dinka nchini humo. Aidha jopo hilo limebaini kuwa wanajeshi walifanya vitendo vya udhalilishaji wa kingono pamoja na vitendo vingine vya kikatili dhidi ya wafanyakazi wa mashirika ya misaada nchini humo katika mji wa Juba mnamo Julai 11, mwaka huu.

Jopo hilo limesema vitendo vilivyofanywa na wanajeshi hao ikiwa ni pamoja na kuiba mali na kufanya uharibifu katika maeneo ya wafanyakazi wa mashirika hayo ya misaada vinaashiria kuwa mashambulizi hayo yaliratibiwa vyema na ngazi za juu za serikali ya nchi hiyo.

Kwa upande mwingine Umoja wa Mataifa umeagiza kufanyike uchunguzi mwingine ili kubaini iwapo wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa walioko nchini humo walishindwa kuwalinda raia ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wa mashirika ya misaada ambao walilazimika kutuma ujumbe kwa njia ya simu kwa wanajeshi hao kwa lengo la kupata msaada.

Sudan Kusini yaendelea kuuziwa silaha

Wakati huohuo katika ripoti yake jopo hilo limedai kuwa mauzo ya silaha kwa jeshi la Sudan Kusini yalikuwa yakiendelea na kutolea mfano wa mauzo ya ndege mbili za kivita chapa L-39 ambapo moja ya ndege hizo ilitumika katika mashambulizi hayo ya mwezi Julai.

Südsudan Einwilligung Sationierung zusätzlicher Blauhelmsoldaten
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Lynch

Serikali ya Rais Salva Kiir imekuwa ikifanya mazungumzo na kampuni moja iliyosajiliwa nchini Lebanon ya Rawmatimpex kwa ajili yakujenga kiwanda kidogo cha kutengeneza silaha nchini humo ingawa matokeo ya mazungumzo hayo bado hayajawa wazi. Imesema ripoti hiyo.

Sudan Kusini ilitumbukia kwa mara ya kwanza katika vita Desemba 2013 wakati Rais Salva Kiir alipomtuhumu aliyekuwa makamu wake Riek Machar kuwa alikuwa akipanga njama za kutaka kufanya mapinduzi.

Mwandishi: Isaac Gamba/ AFPE

Mhariri :Gakuba Daniel