Shambulizi latokea Karibu na msikiti Madina
5 Julai 2016Mshambuliaji huyo kwenye msikiti wa Mtume mjini Madina alijiripua baada ya polisi kuanza kumshuku na kumsogelea akiwa ndani ya gari lake, kwenye sehemu ya kuegesha magari mkabala na Msikiti wa Mtume, ambao ni wa pili katika sehemu takatifu sana kwenye ulimwengu wa kiislamu. Mbali na maafisa wanne waliouawa katika mripuko huo, wengine watano walijeruhiwa.
Huo ulikuwa mripuko wa tatu katika muda wa siku moja, takribani saa 24 tu kabla ya kumalizika kwa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan. Awali, mshambuliaji mwingine aliulenga ubalozi mdogo wa Marekani katika mji wa Jeddah ulio kwenye Bahari ya Sham, na mwingine aliulenga msikiti wa washia katika mji wa Qatif.
Tovuti ya habari ya Sabq ambayo iko karibu na Ufalme wa Saudi Arabia imesema mshambuliaji kwenye msikiti wa mtume huko Madina aliwalenga maafisa wa usalama wakati walipokuwa wakila futari.
Sala kama kawaida
Kituo cha televisheni cha al-Arabiya kinachomilikiwa na Saudi Arabia kimeripoti kuwa waumini walishiriki sala kama kawaida katika msikiti huo uliolengwa, na kilionyesha video ambazo kimesema ni za waumini hao, wakijazana katika ukumbi ulio mbele ya msikiti huo.
Kuna ripoti zinazokinzana kuhusu wahanga wa shambulizi kwenye msikiti wa washia wa Qatif, ambao mwezi Mei mwaka 2015 ulikumbwa na shambulizi jingine baya la kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS ambalo liliwauwa watu 22.
Tovuti ya Sabq imesema washambuliaji wawili walijiripua baada ya kushindwa kuufikia msikiti huo wa Faraj al-Omran, lakini msemaji wa wizara ya mambo ya ndani Jenerali, Mansour al-Turki alisema alikuwepo mshambuliaji mmoja, na kuongeza kuwa maiti tatu zilikuwa eneo la mripuko.
Mashambulizi kwenye misikiti ya Madina na Qatif yalitokea kwa wakati mmoja, wakati watu walipokuwa wakijiandaa kufuturu.
Dola la kiislamu lashukiwa kuhusika
Ingawa bado hakuna kundi lililodai kuhusika na mashambulizi hayo, kundi la IS ambalo Jumapili liliuwa watu 213 katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad, limekuwa likilaani vikali serikali ya Saudi Arabia, inayoongozwa na familia ya kifalme.
Wizara ya mambo ya ndani ya Saudi Arabia imesema inashuku mashambulizi hayo yalifanywa na wapiganaji wa jihadi, na kulaani wale iliosema wamepotea njia, maneno ambayo aghalabu hutumiwa kumaanisha kundi la IS na mtandao wa al-Qaida.
Wizara ya mambo ya ndani ilimtambulisha shambuliaji aliyelenga ubalozi mdogo wa Marekani mjini Jeddah kama Abdullah Qalzar Khan, raia wa Pakistan aliyefanya kazi ya kuendesha gari, ambaye ameishi mjini Jeddah kwa muda wa miaka 12 pamoja na mkewe na wazazi wake.
Iran, ambayo ni hasimu wa Saudi Arabia katika Kanda ya Mashariki ya Kati imeyalaani mashambulizi hayo, ikisema magaidi wamekiuka miiko yote, na kutaka wasuni na washia waungane kuwapiga vita.
Mwandishi: Daniel Gakuba/afpe/dpae
Mhariri: Grace Patricia Kabogo