Shauku yaongezeka
11 Septemba 2015Uamuzi wa Umoja wa vyama vya kandanda barani Ulaya UEFA wa kuongeza idadi ya timu katika mashindano ya kombe la mataifa ya Ulaya miaka sita iliopita ulikosolewa na wengi. Lakini leo hii mamilioni ya mashabiki wa soka barani Ulaya wanafurahia uamuzi huo, wakati huu ikiendelea michuano ya kuwania tiketi ya kucheza fainali za mashindano hayo 2016. Lilipotolewa zao la kuongeza idadi ya timu kutoka 16 hadi 24, gazeti moja la Uingereza lilitaja fikra hiyo kuwa ni wazo la kiwenda wazimu, wakati chombo kimoja cha utangazaji cha kimataifa kikilitaja kuwa ni wazo baya, ambalo litahujumu ubora wa utaratibu wa kuwa na timu 16, ambao umekuweko tokea 1996.Lakini ukijaribu sasa kuwaambia mashabiki wa Iceland kwamba ilikuwa fikra mbaya hawatokubaliana na wewe hata kidogo. Pendekezo la timu 24 lilitolewa na Mfaransa Michel Platini, Rais wa Umoja wa vyama vya kandanda barani Ulaya-UEFA .
Mnamo wiki hii Platini aliliambia Shirika la habari la Reuters kwamba amefurahishwa kuona mfumo huo umekuwa na tija kwe timu za taifa barani humu, kwani kumekuweko na ushindani mkubwa katika makundi mbali mbali yanayowania kufuzu, kiwango cha juu cha soka na shauku kubwa katika mataifa kadhaa ambayo hayakupata kushiriki mashindano makubwa.
Iceland nchi ndogo kabisa ya wakaazi duniani wakiwa karibu 350,000, imefanikiwa kwa mara ya kwanza katika historia kupata tiketi ya kucheza fainali za kombe la Ulaya mwaka ujao.Iceland iko nafasi ya 100 katika orodha ya timu bora duniani kwa kuzingatia kiwango cha soka , ya Shirikisho la Kandanda la Kimataifa FIFA. Nyengine ni Wales inayoweka matumaini ya kufuzu ambapo pindi ikifanikiwa itakuwa ni mara ya kwanza inashiriki katika fainali za mashindano makubwa ya kandanda tokea kombe la dunia 1958. Ireland ya kaskazini ambayo imeshindwa kufuzu katika mashindano yote tangu kombe la dunia nchini Mexico 1986, pia imo ukingoni kukaribia kuwaletea furaha mashabiki wake.
Kukiwa kumesalia duru mbili za mwisho, England, Austria, Iceland na Jamhuri ya Cheki zimeshafanikiwa kwenda Ufaransa msimu wa kiangazi mwakani, wakati timu nyengine 31 za taifa zinaendelea kuumana na 18 zikiwa zimeshatolewa.Mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Sweden Stefan Schwatz ambaye kilabu alizozichezea ni pamoja na Benfica , Arsenal ,Fiorentina na Valencia pia anaipongeza Iceland ambayo mwalimu wake ni aliyekuwa mwalimu wa zamani wa timu ya taifa ya Sweden akiwemo Schwatrz kama mchezaji wakati huo, Lars Lagerbeck. Schwarz anasema mfumo wa kuwa na timu 24 umezipa nafasi nchi nyengine ziweze nazo kufanikiwa na kupata ujuzi na maarifa zaidi.
Uholanzi ambayo ilifikia hatua ya nusu fainali katika Kombe la dunia mwaka jana nchini Brazil, inakabiliwa na kitisho cha kutofanikiwa kwenda Ufaransa na inahitaji matokeo bora michuano iliosalia ili iweze kufanikiwa. Uholanzi ilitandikwa kwa mshangao na Uturuki mabao 3-0 mapema wiki hii. na kocha mpya Danny Blind aliyechukua nafasi baada ya Guus Hiddink kujiuzulu anaonekana kukabiliwa na kibarua kigumu. Mabingwa wa Kombe la dunia Ujerumani na wa Ulaya-Uhispania, wanaongoza makundi yao na wanatarajia kufanikiwa, ingawa hakuna aliye na uhakika hadi sasa.
Kuna timu nyengine zinazojiwekea matumaini, kama Albania, Israel, Estonia na Hungary iliotamba wakati mmoja katika soka la dunia na ambayo sasa iko nafasi ya 37 katika orodha ya dunia. Zote zinawania alau kuingia katika kundi la mtowano baadae, pindi zitashindwa kufuzu kucheza fainali hizo za kombe la mataifa ya Ulaya moja kwa moja kupitia makundi yao. Kwa jumla wazo la kuongezwa idadi ya timu katika fainali za mashindano hayo, kutoka 16 hadi 24, linaonekana sio tu limewapa nafasi wengine , lakini pia limeongeza shauku miongoni mwa mashabiki wa soka barani Ulaya.
Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman,rtre
Mhariri: Gakuba Daniel