1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya kupambana na Malaria yaadhimishwa

25 Aprili 2016

Leo (25.04.2016) ni siku ya kimataifa ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, WHO, mataifa sita ya Afrika huenda yakautokomeza kabisa ugonjwa huo ifikapo mwaka 2020.

https://p.dw.com/p/1Ic9n
Simbabwe Moskitozelt
Neti iliyonyunyiziwa dawa ya kuua mbu imekuwa na mchango mkubwa katika kuziia maambukizi ya malariaPicha: DW/P. Musvanh

Leo ni siku inayozipa fursa nchi mbalimbali duniani kuonyesha ufanisi wao katika kuudhibiti ugonjwa huu na kuziunganisha jitihada tofauti tofauti katika ulimwengu unaoendelea kubadilika.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni "Tokomeza Malaria Kabisa". Kufuatia ufanisi mkubwa uliopatikana chini ya malengo ya maendeleo ya milenia, ni muhimu kuuendeleza ufanisi huu na kuutokomeza kabisa ugonjwa wa malaria chini ya malengo ya maendeleo endelevu. Kauli mbiu hiyo inaenda sambamba na lengo la kuwa na ulimwengu usio na malaria lilijumuishwa katika mkakati wa kiufundi wa kimataifa kwa ajili ya malaria 2016 hadi 2030, ulioidhinishwa Mei mwaka uliopita na baraza kuu la Afya duniani. Mkakati huo unalenga kupunguza kwa kiwango kikubwa maambukizi ya malaria ulimwenguni katika kipindi cha miaka 15 ijayo.

Kwa mujibu wa ripoti kuhusu malaria ya shirika la afya duniani, WHO, mwaka 2015, visa vya maambukizi ya malaria na vifo kutokana na ugonjwa huo vilipungua tangu mwaka 2000. Ufanisi huenda ulipatikana kupitia utanuzi wa vifaa na nyenzo za kuzuia na kutibu malaria, kama vile neti za mbu zilizonyunyiziwa dawa, kupima malaria na utoaji wa dawa ya kuzuia ugonjwa huo.

Nchi za Afrika kuwa huru kutokana na malaria

Nchi sita za Afrika, zikiwemo, Algeria, Botswana, Cape Verde, Comoro, Afrika Kusini na Swaziland, huenda zikawa huru kutokana na malaria ifikapo 2020. Mojawapo ya malengo ya mpango wa shirika la afya duniani WHO wa kupambana na malaria ni kuutokomeza ugonjwa huo katika nchi karibu 10 kufikia mwisho wa muongo huu. Shirika hilo linakadiria jumla ya nchi 21 duniani ziko katika nafasi nzuri ya kulifikia lengo hilo, zikiwemo nchi sita kutoka Afrika, bara ambalo linakabiliwa na athari kubwa kutokana na malaria.

Malaria Kind
Msichana mdogo akipimwa malaria, Sittwe, jimbo la Arakan, MyanmarPicha: Getty Images

Nchini Afrika Kusini lengo la kuuangamiza ugonjwa wa malaria ni la kitaifa, huku visa 11,700 vya maambukizi vikirekodiwa mwaka 2014, kutoka 64,000 mwaka 2000. Visa vingi viliripotiwa katika maeneo yanayopakana na Swaziland, Zimbabwe na Msumbiji.

Mataifa mengine yanayoaminiwa yanaweza kulifikia lengo hili ni China, Malaysia na Korea Kusini, na nchi nane za Amerika Kusini - Costa Rica, Belize, El Salvador, Mexico, Argentina, Paraguay, Ecuador na Suriname. Saudi Arabia,Iran, Oman, Sri Lanka, Bhuran, Timor Leste na Nepal pia zimetajwa kama nchi zinazoweza kulifikia lengo la kutokomeza kabisa malaria.

Ulaya, Asia ya Kati na Caucasus ni maeneo yaliyotokomeza malaria mwaka uliopita kwa mujibu wa ripoti ya WHO iliyochapishwa mapema mwezi huu. Watu milioni 214 waliambukizwa malaria mwaka jana ambapo watu 438,000 walikufa kutokana na ugonjwa huo, kwa mujibu wa shirika hilo.

Ripoti ya WHO imesema vifo tisa kati ya kumi vilivyosababishwa na malaria mwaka uliopita vilitokea Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara.

Changamoto kubwa bado zingalipo

Kimataifa watu bilioni 3.2, ikiwa ni karibu nusu ya idadi ya wakazi duniani, wako katika hatari ya kuambukizwa malaria. Mwaka uliopita kulikuwa na visa vipya milioni 214 vya maambukizi ya malaria na vifo 438,000, hususan katika nchi za Afrika, kusini mwa jangwa la Sahara. Mamilioni ya watu bado hawatathmini huduma wanazohitaji kuzuia na kutibu malaria.

Siku ya Kimataifa ya mapambano dhidi ya malaria inatoa fursa ya kila mwaka kuangazia maendeleo katika kudhibiti ugonjwa wa malaria na kuahidi kuendelea kuwekeza na kuchukua hatua kuharakisha ufanisi dhidi ya ugonjwa huu hatari. Ili kufikia malengo ya mkakati wa kimataifa dhidi ya malaria, uwekezaji wa kila mwaka kwa ajili ya kudhibiti malaria utahitaji kuongeza mara tatu viwango vya sasa, kufikia dola bilioni 8.7 kila mwaka kufikia mwaka 2030.

Insektizid DDT gegen Malaria-Erreger versprüht
Mtaalamu kinyunyiza dawa ya kuua mbu, Jozini, Afrika KusiniPicha: picture-alliance/dpa

Huku juhudi za kuzuia Malaria zikiwa zimeshika kasi katika miaka iliyopita, kupungua kwa ufadhili wa fedha kunahatarisha kukwamisha ufanisi huo, hususan katika bara la Afrika, ambako mataifa yanakabiliwa na mapengo makubwa ya ufadhili. Mpaka ulimwengu utakapopata njia ya kupunguza mapengo hayo na nchi zinazokabiliwa sana na malaria zitakapokuwa na raslimali na msaada wa kiufundi zinaouhitaji kuitekeleza kikamilifu mipango ya kupambana na ugonjwa huo, kuzuka kwa malaria kutasababisha maisha ya watu wengi kuangamia.

Uwekezaji na ushirikiano mkubwa vimesababisha ufanisi mkubwa dhidi ya malaria katika kipindi cha miaka 15 iliyopita. Vifo kutokana na ugonjwa huo vimepungua kwa asilimia 60, huku maisha ya watu milioni 6.2 yakiokolewa tangu mwaka 2000. Malaria sio tena ugonjwa unaoongoza kwa kusababisha vifo vya watoto barani Afrika.

Kuudhibiti ugonjwa wa malaria ni muhimu katika kuutokomeza umaskini na kuimarisha afya ya akina mama wajawazito na mtoto. Maisha yaliyookolewa kutokana na malaria yanakadiriwa kuwa asilimia 20 ya ufanisi wote katiak kupunguza vifo vya watoto katika mataifa ya Afrika kusini mwa jangwa la Sahara tangu mwaka 2000. Juhudi za kuzuia malaria wakati wa ujauzito pekee zimeepusha vifo vya watoto wachanga 94,000 kati ya mwaka 2009 na 2012.

Kunapokuwa na maambukizi machache ya malaria ina maana jamii zinakuwa na afya bora, idadi ya watoto wanaokwenda shule inaongezeka, watu wanaweza kufanya shughuli zao na kuzalisha bidhaa na uchumi huimarika. Kuungamiza ugonjwa wa malaria ni muhimu sana katika kuyafikia malengo endelevu na lazima libakie kuwa suala la kipaumbele kwa jumuiya ya maendeleo ya kimataifa.

Wakati ulimwengu unapoadhimisha siku ya mapambano dhidi ya Malaria, pana haja ya kuendeleza uwekezaji, ari ya kisiasa na ubunifu kuhakikisha ufanisi unaendelea kuwepo dhidi ya ugonjwa huo.

Kutokomeza malaria kutaufanya ulimwengu kuwa mahala pazuri pa kuishi, salama kwa vizazi vijavyo na kuwawezesha mamilioni ya watu kufikia malengo yao kimaisha.

Mwandishi:Josephat Charo/afpe/who.int/

Mhariri: Grace Patricia Kabogo