Wakimbizi wahudumiwe ipasavyo
21 Juni 2016Tuanzie lakini na siku ya wakimbizi duniani. Gazeti la mjini Frankfurt Oder,"Märkische Oderzeitung" linachambua sababu zinazowafanya watu kuyapa kisogo maskani yao na kuandika: " Ukuaji wa kasi wa kiuchumi na kupungua idadi ya wakimbizi,vina sababu yake;Inaitwa nchi iliyoshindwa. Watu wanatokea katika nchi ambako miundo mbinu imevurugika kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe. Wanakimbia maovu na matumizi ya nguvu ya wafuasi wa itikadi kali. Hayo hayatoshi.Makampuni ya silaha ya Ujerumani yanaziuzia silaha nchi mfano wa Saud Arabia. Nchi ambayo kwa muda wa mwaka sasa inaihujumu kwa mabomu Yemen na kusababisha kuongezeka idadi ya wakimbizi. Na sisi tufanye kana kwamba hatuhusiki na yote hayo? Ulaya si kisiwa. Sawa na tunavyohitaji mafuta ya Saud Arabia au maadini ya bara la Afrika ili kuendeleza kiwango cha maisha yetu,ndivo ambavyo Ulaya,kwa masilahi yake wenyewe,haibidi kupalilia vita vya wenyewe kwa wenyewe, badala yake inapaswa iwahudumiwe wakimbizi kule kule walikotokea,iwapatiwe makaazi yanayostahiki hadi watakapoweza kurejea nyumbani. Kwasababu njia ya kuja Ulaya hata bila ya ukuta,inauwa.
Urusi ibembelezwe,lakini isichokozwe
Mbali na wakimbizi vikwazo vya Umoja wa ulaya kwa Urusi pia vinawakosesha usingizi baadhi ya wanasiasa wa Ujerumani.Gazeti la "Mitteldeutsche Zeitung" linaandika: "Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amevunjika moyo kwasababu,anaona anashindwa kushinikiza si ndani ya serikali kuu ya Ujerumani na wala si miongoni mwa washirika wa magharibi,uhusiano ukwamuliwe hatua baada ya hatua pamoja na Urusi. Bila shaka siasa ya uwiano inayofuatwa na wizara yake si mbaya-inadhihirisha maamuzi yaliyofikiwa yanaheshimiwa,lakini pia anatambua maamuzi mengine hayawezi kudumu milele.Urusi ni nchi muhimu duniani. Nchi za magharibi zinatakiwa zimnyoshee mkono rais wa Urusi apate kugutuka. Kwa kila hali lakini asichokozwe. Watangulizi wake katika ikulu ya Urusi-Kremlin,walioanzisha pamoja na Willy Brandt sera inayozingatia uhusiano pamoja na nchi za ulaya ya mashariki ,mashuhuri kwa jina la Ostpolitik,hawakuwa wanademokrasia waliobobea. Kama mbinu za Steinmeier zinachochewa na siasa ya ndani? Hakuna ajuaye lakini hata kama ndio hivyo,ubaya uko wapi,hata siasa ya nje ya Willy Brandt ililazimika kuzilenga serikali mpya.
Karata zatachanganywa upya mwaka 2017
Mada yetu ya mwisho magazetini inahusiana na wito wa mwenyekiti wa chama cha Social Democratic SPD,Sigmar Gabriel kutka vyama vya mrengo wa kushoto vishikamane kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.Gazeti la "Rhein-Zeitung" linaandika: "Washirika wa Vyama ndugu vya CDU/CSU na wale wa SPD wameshachokana. Kila upande umeshatangaza dhamiri ya kutoendelea na serikali ya muungano baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2017. Hilo ni jambo linaloeleweka,kwamba hakuna tena miradi ya pamoja na kwamba pande zote mbili kiwango cha umaarufu wao kinazidi kuporomoka. Kuna uwezekano mkubwa, msimu wa mapukutiko mwaka 2017 ukakosekana msingi wa kuunda serikali ya muungano. Lakini wakati huo watu wangebidi waangaliane uso kwa macho.
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Mohammed Khelef