Sintofahamu yaendelea Italia kuhusu serikali mpya
30 Mei 2018Carlo Cottarelli ambaye aliteuliwa na Rais Sergio Mattarella mapema wiki hii kuunda serikali ya mpito kuelekea uchaguzi mpya, amefanya mazungumzo na rais huyo katika Ikulu ya Quirinale mjini Roma, baada ya uteuzi wake kushindwa kutuliza wasiwasi katika masoko ya fedha na mitaji. Hakusema chochote wakati alipokuwa akiingia katika makazi ya rais, na wala ofisi ya rais haijatoa maelezo ya kina kuhusu mazungumzo baina ya viongozi hao.
Cottarelli ambaye amekabidhiwa jukumu la kuandaa uchaguzi mpya mwezi Julai ameshindwa kupata ushirikiano wa vyama vikubwa, hata ule wa kumruhusu kuunda serikali ya kuiongoza nchi hadi wakati wa uchaguzi.
Badala yake vyama hivyo vinamtaka Rais Mattarella kulivunja bunge na kuitisha uchaguzi mpya mara moja, ambao unapendekezwa kufanyika tarehe 29 Julai, kipindi cha miezi isiyotimia minne tangu uchaguzi wa Machi 4 ambao haukubainisha mshindi wa wazi.
Tetesi juu ya juhudi za maridhiano
Baadhi ya vyombo vya habari vya Italia vinazungumzia uwezekano wa kupatikana muafaka kati ya rais na vyama vyenye misimamo mikali ya kizalendo na vinavyopinga Umoja wa Ulaya; kile cha League na Vuguvugu la Nyota Tano. Tofauti kubwa iliibuka baada ya hatua ya Rais Mattarella kukataa pendekezo la vyama hivyo, la Paolo Savona kuwa waziri wa uchumi. Savona mwenye umri wa miaka 81 anajulikana kwa msimamo shupavu dhidi ya kushiriki kwa Italia katika ukanda wa sarafu ya euro.
Kiongozi wa Vuguvugu la Nyota Tano Luigi di Maio amesema wako tayari kuzungumza na pande zote kupata suluhisho la mgogoro unaoighubika nchi.
''Nataka kusema mambo mawili hapa, pamoja na kutaka uchaguzi wa mapema iwezekanavyo, utashi wetu wa kufanya kazi na kila upande, rais akiwemo, unabaki pale pale, huku tukiendelea kushikilia msimamo wetu ili kuweza kuumaliza mgogoro tunaoushuhudia.'' amesema Di Maio na kuongeza kuwa si wao walioleta mgogoro huu.
''Kama masoko yameingiwa na wasiwasi kwamba serikali yetu itaiondoa Italia katika umoja wa sarafu ya Euro, ni kwa sababu kuna mtu ameyaambia serikali hii mpya inataka kuondoka katika sarafu ya euro.'' ameongeza.
''Ndugu wa Italia kushirikishwa katika serikali?
Wakati Carlo Cottarelli akijaribu kuunda serikali yake ya mpito, zipo taarifa kuwa maafisa wa Vuguvugu la Nyota Tano na chama cha League wanajaribu kukubaliana juu ya mtu mpya wanayeweza kumpendekeza katika wadhifa wa waziri wa fedha badala ya Paolo Savona aliyeleta mtafaruku. Taarifa hizo zimedai kuwa vyama hivyo vinatafakari kukishirikisha chama kingine chenye sera kali za mrengo wa kulia cha ''Ndugu wa Italia'' katika serikali.
Ikiwa uchaguzi mpya utaitishwa, suala kubwa la kampeni litakuwa pendekezo la Paolo Savona la kutaka Italia iondoke katika umoja wa sarafu ya euro, na uchunguzi wa maoni ya wapiga kura unaonyesha kuwa vyama vinavyopinga mkondo wa utawala uliozoeleka, vitajiimarisha zaidi.
Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre, ape
Mhariri: Grace Patricia Kabogo