SOFIA:Wahudumu wa afya wasamehewa na rais wa Bulgaria
24 Julai 2007Wahudumu sita wa afya wa Bulgaria waliohukumiwa kifungo cha maisha na mahakama nchini Libya wamesamehewa na rais mnamo walipowasili nchini mwao,Bulgaria.Hatua hiyo inawaweka huru baada ya kuzuiliwa jela kwa miaka 8 nchini Libya.
Wauguzi 5 na daktari mmoja waliwasili mjini Sofia wakiwa safarini na mkewe Rais Nikolas Sakorzy wa Ufaransa Bi Cecilia Sarkozy pamoja na kamishna wa mambo ya nje wa umoja wa Ulaya Benita Ferrero Waldner. Jamaa na marafiki waliwalaki wahudumu hao kwenye uwanja wa ndege wa Sofia.Umoja wa Ulaya unatangaza kurejesha uhusiano na Libya baada ya kuwaruhusu wahudumu hao kurejeshwa Bulgaria.Jose Manuel Barosso ni kamishna wa Tume ya Ulaya
''Tuna imani kuwa tutarejesha uhusiano wetu na nchi ya Libya.Uhusiano kati yetu uliathiriwa na suala hili ambalo lilikuwa halijapata ufumbuzi.Nadhani wanaelewa kuwa Umoja wa Ulaya ni kitu kimoja na tunajali maslahi ya wenzetu barani Ulaya.''
Libya iliwashtaki wahudumu hao kwa kuwaambukiza zaidi ya watoto 400 virusi vya Ukimwi na kuwazuia jela tangu mwaka 99.Wahudumu hao walio na umri kati ya miaka 41 na 54 wanakanusha mashtaka hayo na kuongeza kuwa waliungama kwasababu ya mateso.Mazungumzo kati ya Umoja wa Ulaya na Libya yalipelekea kuachiwa kwa wahudumu hao.