Solskjaer kuimarisha kikosi cha ManU
17 Agosti 2020Manchester United ya Uingereza imefurushwa katika awamu ya nusu fainali na Seville ya Uhispania baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 jana Jumapili. Kocha wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer amesema kuwa anapanga kuimarisha kikosi chake kabla ya msimu ujao kuanza kufuatia kipigo hicho ambacho hakukitarajia katika mchezo wa nusu fainali mjini Cologne jana Jumapili.
Baada ya kuangukia pua mara mbili katika awamu ya nusu fainali katika kuwania vikombe msimu huu , United ilikuwa inalenga kusongambele hatua moja zaidi kwa kufikia fainali ya Europa League Ijumaa ijayo.
Walionekana mwanzoni kuwa wanaelekea kufanya hivyo baada ya Bruno Fernandes kuweka mpira wavuni kwa penalti ikiwa ni penalti yao ya 22 ya msimu katika dakika ya tisa ya mchezo katika uwanja wa Rhine Energie mjini Cologne. Hata hivyo , magoli kutoka kwa winga wa Uhispania Suso na mchezaji wa zamani wa Newcastle United Luuk de Jong yalihakikisha mabingwa mara tano wa Europa League Seville watakumbana na ama Inter Milan ama Shaktar Donestsk katika fainali, wakati Man United ikimaliza msimu bila ya kupata taji.
Mfungaji wa bao la ushindi la Seville Luuk de Jong aliongoza kumwagia sifa mlinda mlango Yassine Bono baada ya kufanya maajabu kuokoa mipira kadhaa ya Manchester United katika mchezo huo wa nusu fainali jana. Kocha wa Seville Julien Lopetegui , ameisifu kwa jumla timu yake kwamba ilicheza kwa moyo mkubwa.
"Tulicheza kwa moyo mkubwa, wachezaji wajiamini, walikimbia. Tuliweza kucheza mpira katika kipindi cha pili na kucheza vizuri zaidi,na kisha goli lilipatikana. Tumefurahi kupata nafasi katika fainali, vijana walifurahi sana, walistahili. Ni kikosi cha aina yake, wanastahili kucheza fainali. Tunafuraha kubwa kuwapa mashabiki wetu kitu cha kufuahia katika wakati huu mgumu. Na sasa tuna ndoto ya kucheza katika fainali. Hatujui nani mpizani wetu , lakini bila shaka itakuwa ngumu zaidi kuliko leo. Tunapaswa kujitayarisha."
Mchezaji aliyetokea katika benchi De Jong aliwasha moto kuwaingiza Seville katika fainali ijayo Ijumaa katika dakika ya 78, lakini ni pale Mmoroco Yassine Bono alipopambana na mashambulizi makali ya United peke yake. Huyu hapa Bono.
"Kama nilivyosema siku iliyopita, najihisi wakati wote kama sehemu ya timu. Kila mara naweka mtazamo wangu katika malengo, nicheze au nisicheze , tushinde ama kushindwa. Kila mara najihisi kama nimo ndani ya boti. Najaribu kufanya kazi yangu, hakuna kingine, tunafahamu kuwa mchezo ni wakati. Baadhi ya wakati unajitokeza na kufanya vizuri. Tulikuwa na wakati mgumu katika mchezo, lakini tumethibitisha kuwa ni timu nzuri, tulikuwa na mpira, tuliwafanya waukimbize na kuniruhusu mimi kupumua kidogo."
Ushujaa aliouonyesha Yassine Bono wa Seville, uliwaacha midomo wazi mashabiki wa kandanda na mashabiki wa Manchester United wanahisi huyo ndie aliyewanyima hata kata ya maji.
Nilizungumza na mwenzangu katika meza ya michezo DW idhaa ya Kiswahili Bruce Amani kuhusu msisimko unaojitokeza katika michezo hii ya mtoano msimu huu ya Champions League na Europa League, nae alikuwa na haya ya kusema.