Somalia: Watu 6 wauawa kwenye shambulio la kujitoa muhanga
2 Septemba 2018Afisa wa polisi kapteni Mohamed Hussein ameliambia shirika la habari la AP kuwa mshambuliaji huyo alijaribu kukivuka kizuizi cha polisi kwa kuliendesha gari lake kwa kasi lakini aliposimamishwa na maafisa wa usalama, ndipo alipolilipua lori hilo karibu na lango la makao makuu ya wilaya ya Howlwadag.
Kwa mujibu wa msemaji wa Meya wa Mogadishu Salah Hassan Omar, askari watatu waliolisimamisha lori hilo waliuawa hapo hapo, wengine watatu waliouawa walikuwa raia.
Taarifa za shirika linalotoa huduma za kuwabeba wagonjwa la Aamin zinaeleza kuwa watu 14 ikiwa ni pamoja na watoto sita, wanahitaji kuangaliwa kwenye kitengo cha watu mahututi. Naibu mkuu wa wilaya Ibrah Hassab Matan ni miongoni mwa watu waliojeruhiwa.
Wengi waliokumbwa katika mkasa huo walikuwa wanafunzi waliokuwemo kwenye Madrasa na polisi imetahadharisha kuwa huenda idadi ya watu waliojeruhiwa ikaongezeka.
Kulingana na afisa wa polisi kapteni Hussein, wanamgambo wa kiislamu wa Al-shabaab kundi linalofungamana na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda wamedai kuhusika na shambulio hilo kupitia kwenye kituo cha radio kinachowapendelea cha Andulus. Kundi hilo mara kwa mara hufanya mashambulizi katika nchi hiyo ya Afrika mashariki.
Jeshi la Somalia linatarajiwa kuchukua majukumu ya kulinda usalama kwenye taifa hilo lililo kwenye Upembe ya Afrika katika miaka ijayo kutoka kwa majeshi ya kulinda Amani ya Umoja wa Afrika licha ya kuwepo wasiwasi kuhusu utayari wa vikosi vya usalama vya Somalia.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hivi karibuni lilipiga kura kwa ajili ya kucheleweshwa zoezi la kuwapunguza askari wa Umoja wa Afrika kuanzia mwezi Oktoba hadi mwezi Februari huku muda wa kukabidhi majukumu ya kulinda usalama kwa vikosi vya Somalia uwe mwezi Desemba mwaka 2021.
Mwandishi: Zainab Aziz/APE/RTRE/AFPE
Mhariri: John Juma