Nchi za ghuba zaombwa kuwapokea wakimbizi zaidi
19 Oktoba 2015Tunataka eneo lote katika ghuba ya Arabuni kushiriki katika kuwapatia msaada wakimbizi, Steinmeier amesema kufuatia mazungumzo na mfalme wa saudi Arabia Salman mjini Riyadh.
Steinmeier , ambaye yuko katika ziara ya siku nne katika eneo hilo la ghuba, amesema hii ni pamoja na kuwachukua wakimbizi. Mataifa tajiri ya ghuba yamekabiliwa na ukosoaji kwa kusita kwao kuwapokea wakimbizi wa Syria.
Mataifa ya ghuba yanasema yamechukua mamia kwa maelfu ya wakimbizi wa Syria tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vianze mwaka 2011, ikiwa ni pamoja na wakimbizi nusu milioni nchini Saudi Arabia na laki moja katika Umoja wa Falme za Kiarabu.
Wakati huo huo maelfu ya wahamiaji wameendelea kumiminika leo katika mataifa ya Balkan, ambako udhibiti mkubwa wa mipaka umesababisha mlundikano wa wahamiaji, wengi wao wakikimbia vita nchini Syria , Iraq na Afghanistan, wakisafiri kupitia Uturuki, Ugiriki na mataifa ya Balkan magharibi, wakiwa na matumaini ya kupata usalama nchini Ujerumani na mataifa mengine ya Ulaya.
Wakimbizi wazidi kuingia Ulaya
Wimbi jipya limeingia Macedonia kutoka Ugiriki mwishoni mwa juma, wakati watu 10,000 wanavuka na kuingia katika nchi hizo katika muda wa saa 24 zilizopita, polisi imesema.
Lakini hali ya wasi wasi imeongezeka zaidi katika njia wanayopitia wakimbizi baada ya Hungary kufunga mpaka wake kwa uzio wa waya, na kusababisha mmiminiko huo wa wahamiaji kuelekea upande wa magharibi kuelekea Slovenia, ambayo nayo imeweka ukomo kwa watu wanaowasili.
Slovenia leo imekataa kuwaruhusu wahamiaji zaidi ya 1,000 wanaowasili kutoka Croatia, wakisema kiwango cha ruhusa ya kuingia kwa siku kimefikiwa.
Hatua hiyo imeongeza hofu ya mkusanyiko mkubwa wa watu, wakati treni iliyowabeba watu 1,800 ikiwasili usiku katika upande wa pili wa mpaka wa Croatia , lakini ni watu 500 tu , wale ambao wanaweza kukabiliwa haraka na matatizo , wengi wakiwa wanawake na watoto, wakiruhusiwa kuvuka mpaka, polisi imesema.
Misururu mirefu
Misururu mirefu pia ilionekana katika upande wa mpaka kati ysa Serbia na Croatia, ambako mamia walilala usiku kucha wakinyeshewa na mvua na baridi kali.
Kansela wa Ujerumani wa Ujerumani amesema tatizo la wakimbizi ni lazima lipatiwe ufumbuzi na mataifa ya Ulaya na jumuiya ya kimataifa.
"Kupambana na wimbi kubwa kabisa duniani la wakimbizi tangu vita vikuu vya pili vya dunia ni tatizo la dunia na linaweza tu kushughulikiwa kwa mtazamo wa pamoja wa mataifa ya Ulaya na dunia kwa jumla."
Lengo la wengi wa wahamiaji hao ni nchi yenye uchumi mkubwa katika Umoja wa Ulaya , Ujerumani, ambayo inatarajia kuwachukua karibu wakimbizi milioni moja mwaka huu, na ambako sera za kansela Angela Merkel za kuweka milango wazi zimezusha shutuma nyingi dhidi yake.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / rtre
Mhariri: Yusuf , Saumu