Sudan Kusini: Raia 16 wauawa kufuatia vita Wau
11 Aprili 2017Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo UNMISS umesema mapigano hayo yalitokana na kuuawa kwa askari wa jeshi la serikali.SPLA waliokuwa wakipiga doria eneo hilo la kaskazini mwa Sudan Kusini. Karibu nusu ya mji huo wa Wau imesalia kimya huku maduka na hata masoko yakifungwa kufuatia tangazo la serikali la kuwataka wenyeji kusalia majumbani mwao. Ujumbe wa UNMISS umesema watu 84 wametafuta hifadhi katika kambi ya kuwalinda raia ya Umoja wa Mataifa huku wengine wapatao elfu tatu wakipewa hifadhi katika kanisa moja la katoliki lililo katika mji huo wa Wau baada ya kuhofia usalama wao. Kwa mujibu wa mmoja wa wakaazi; idadi ya waliofariki huenda ikiwa juu kuliko ilivyoripotiwa na waliolengwa hasa ni kutoka makabila ya wachache ya Jur na Balanda wanaodaiwa kuwaunga mkono waasi. Mji huo wa Wau umo katika eneo ambalo limeshuhudia mara kadhaa ubadilishanaji udhibiti kati ya vikosi vya serikali na waasi wanaomuunga mkono aliyekuwa makamu wa rais Riek Machar tangu kuzuka mapigano ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2013. Hata hivyo mji wenyewe miaka yote umesalia chini ya usimamizi wa wanamuuunga mkono rais Salva Kiir. Ujumbe wa UNMISS umesema wiki iliyopita kuwa vikosi vya serikali vilisafirisha vifaa vyao na magari ya kijeshi katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi kusini mashariki mwa mji huo wa Wau.
Taarifa zinazohitilafiana
Msemaji wa kijeshi Santo Choi amesema mapigano hayo yanatokana vikosi vyake kuanzisha harakati za kuwatimua waasi kutoka eneo hilo ambalo ni ngome yao kwa muda mrefu.Nae msemaji wa waasi William Deng amesema vurugu za sasa zilitokana na uvamizi waliofanya dhidi ya vikosi vya serikali siku ya jumapili ambapo 35 miongoni mwao walifariki.Katika kulipiza kisasi msemaji huyo wa waasi amesema majeshi ya serikali yalirejea katika mji huo wa Wau ambapo walifanya msako wa nyumba kwa nyumba na kuwaua raia 50. Taarifa hizo kutoka kwa serikali na waasi bado hazijathibitishwa. Viongozi wa South Sudan walipigania uhuru miongo kadhaa, lakini tangu kuupata uhuru huo mwaka 2011 mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yalianza mwaka 2013 kufuatia mapambano ya kuwania uongozi kati ya rais Kiir na aliyekuwa makamu wake Riek Machar. Watu wapatao millioni 1.7 wametoroka Sudan Kusini tangu taifa hilo kutumbukia katika vita huku wengine millioni 1.9 wakisalia wakimbizi wa ndani. Mapigano hayo pia yamesababisha ukame na kuchochea mgogoro wa kibinadamu.
Mwandishi:Jane Nyingi/AFPE
Mhariri:Iddi Ssessanga