Sudan kusini yaondoa kikwazo kwa serikali ya Umoja wa Taifa
15 Februari 2020Kikwazo hicho kilichokuwa kinazuwia uundwaji wa serikali ya Umoja wa Kitaifa ni suala nyeti kisiasa juu ya idadi ya majimbo.
Rais Salva Kiir amesema baada ya mkutano na hasimu wake Riek Machar jana Ijumaa (14.02.2020) ameamua kuirejesha nchi hiyo changa duniani kuwa na majimbo 10 pamoja na maeneo matatu ya utawala, na kupunguza suala "kuu la mvutano" wakati nchi hiyo ikijitoa kutoka katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Makubaliano hayo yatasaidia kuipeleka nchi hiyo kuvuka "mzozo huu usiokuwa na sababu", rais amesema, akiuita muafaka huo kuwa ni "moja katika maamuzi magumu yanayoumiza ambayo hajawahi kuyafanya."
Mbinyo wa kimataifa kutoka Marekani na mataifa mengine umekuwa ukiongezeka dhidi ya Kiir na Machar kufikia muda wa mwisho wa Februari 22 kujiunga pamoja katika serikali ya Umoja wa Kitaifa. Muda huo wa mwisho umerefushwa mara mbili katika mwaka mmoja uliopita. Machar atarejea kama makamu wa rais wa Kiir, jukumu ambalo mara mbili zilisababisha mzozo.
Marekani, ambayo ni mfadhili mkuu wa misaada ya kiutu nchini Sudan kusini, ilichukua hatua muhimu katika wiki za hivi karibuni za kuweka vikwazo kwa makamu wa kwanza wa rais wa Kiir, Taban Deng Gai.
Utaratibu wa usalama bado ni suala gumu
Masuala magumu bado yanaendelea kuwapo, ikiwa ni pamoja na utaratibu wa usalama ambao ni pamoja na kuunganisha maelfu ya wanajeshi wa zamani waliokuwa wakipigana kuwa jesho moja la taifa.
Mchakato huo umeshuhudia uchelewesho mara kadhaa.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka mitano, ambavyo vilizuka miaka miwili tu kufuatia uhuru wa nchi hiyo kutoka Sudan, vimeuwa watu 400,000 na mamilioni kukimbia makaazi yao.
Uchumi wa nchi hiyo umevurugika na karibu nusu ya nchi hiyo imekuwa katika mzozo mkubwa wa njaa kali.
Idadi ya majimbo limekuwa suala la kubishaniwa na kuleta mivutano kwa miaka kadhaa. Makubaliano ya amani ya mwaka 2015 yaliyoshindwa yaliongeza idadi ya majimbo kutoka 10 hadi 32. Hadi sasa, serikali imesisitiza kuwa na idadi hiyo, wakati upinzani unaoongozwa na Machar ulitaka mbadala wa majimbo 23 ama 10.
Wiki moja iliyopita, wakati viongozi wa kanda wakiweka mbinyo mpya, Kiir aliomba kuongezewa muda zaidi kupata ushauri kwa watu nyumbani kuhusu suala hilo. Maelezo ya tangazo la Jumamosi sasa yatapelekwa kwa viongozi wa bodi ya kanda ya Afrika mashariki pamoja na upande wa Machar.