Sudan Kusini yapinga pendekezo la wanajeshi zaidi
12 Agosti 2016Sudan Kusini hapo jana ilipinga pendekezo la Marekani kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kupeleka wanajeshi elfu 4 zaidi nchini humo kusaidia katika udumishaji amani na kusema hatua hiyo itahujumu uhuru wa nchi hiyo na kutishia kuirejesha nchi hiyo katika enzi za ukoloni.
Mwezi uliopita, serikali hiyo ilisema kuwa itaruhusu kupelekwa kwa vikosi vya kijeshi mjini Juba baada ya mapigano kati ya majeshi ya Rais Salva kiir na wanajeshi wanaomuunga mkono mpinzani wake aliyekuwa makamu wa Rais Riek Machar kusababisha vifo vya mamia ya watu mjini humo.
Matakwa ya Sudan Kusini
Lakini hapo jana waziri wa habari wa Sudan Kusini Michael Makuei alisema kuwa jeshi hilo linapaswa kuwa huru badala ya chini ya amri ya Umoja wa Mataifa. Makuei alisema kuwa hatua ya Marekani ya kuilazimu nchi hiyo kukubali wanajeshi hao zaidi ni hatua ya kibeberu.
Chini ya pendekezo hilo la Marekani, wanajeshi hao wa ziada watakuwa chini ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa Sudan Kusini UNMISS,lililo na wanajeshi takriban elfu 12.
Shutuma za Sudan Kusini
Sudan Kusini imeishutumu UNMISS kwa kushindwa kuwalinda raia wa nchi hiyo. Kulingana na balozi wa Marekani nchini Sudan Kusini, Molly Phee, pendekezo hilo la Marekani linaambatana na matakwa ya jumuiya ya ushirikiano wa kimaendeleo wa nchi za mashariki na pembe ya Afrika IGAD na Sudan Kusini ni mwanachama wa IGAD.
Baraza la usalama litapiga kura hapo kesho kuhusu pendekezo hilo la iwapo kutumwe wanajeshi zaidi Sudan Kusini au la. Hayo yajiri huku Umoja wa Mataifa ukisema takriban raia 70,000 wa Sudan Kusini walilazimika kutorokea nchi jirani ya Uganda baada ya mapigano kuzuka upya nchini humo mwezi uliopita.
Mwandishi. Tatu Karema, AFPE; AP
Mhariri: Caro Robi