Sudan Kusini yashindwa kulipa mishahara ya watumishi
10 Mei 2022Kipato kikubwa cha taifa hilo ambacho ni fedha zinazotokana na sekta ya usafirishaji mafuta kimeelekezwa kulipa mikopo ya taifa hadi mwaka 2017.
Wafanyakazi wanaodai mishahara inajumuisha maafisa wa vikosi vya usalama, madaktari na manesi. Hayo ni kulingana na taarifa iliyotolewa na waziri wa fedha wa Sudan Kusini Agak Achuil.
"Sababu ya kwanini hawalipwi ni kwamba mapato ya mafuta yanatengwa kulipa mikopo iliyochukuliwa kabla na kugharamia vipaumbele vingine vya serikali" amesema waziri Achuil alipozungumza na waandishi wa habari kwenye mji mkuu wa taifa hilo, Juba.
Amesema serikali itatenga fedha za mapato ya mafuta zitakazopatikana mwaka 2028 na kuendelea ili kulipa madeni ya mishahara ya mwaka huu. Waziri huyo amehoji "Wapi nitapata fedha ikiwa mafuta tayari yameuzwa hadi mwaka 2027?"
Kwanini mapato ya mafuta hayainufaishi Sudan Kusini?
Hivi karibuni wizara ya fedha ililipa madai ya mishahara ya mwezi Novemba na Disemba lakini hivi sasa inadaiwa malimbikizo ya mshahara kwa miezi minne ya kwanza ya mwaka 2022.
Serikali ya rais Salva Kiir inategemea mapato ya mafuta kulipa mishahara na kufadhili miradi mingine ya maendeleo. Mapato ya ndani hayatoshi kugharamia matumizi ya serikali ikiwemo mishahara ya watumishi wa umma.
Serikali imekuwa ikikopa fedha kwa kiwango kikubwa kwa kutumia mafuta kama amana. Mwaka 2019 iliridhia kutenga mapipa 10,000 kwa siku kama malipo kwa kampuni za kichina zinazojenga barabara kwenye taifa hilo.
Hata hivyo baadhi ya matumizi yanaonekana kuwa anasa. Uamuzi wa mwaka 2018 wa kuwapatia wabunge 400 wa nchi hiyo kila mmoja mkopo wa dola 40,000 ili kununua magari binafsi ulikosolewa vikali kwenye taifa ambalo wafanyakazi wengi wa serikali wanaishi maisha duni.
Wafanyakazi wa sekta ya afya ni miongoni mwa wale wanaolipwa ujira mdogo sana. Wengi ya mauguzi na wakunga wanalipwa chini ya dola 100 kwa mwezi.
Hali ya maisha inazidi kuwa ngumu kwa watumishi
Baadhi ya watumishi wa umma waliozungumza na shirika la habari la Associated Press wamesema imekuwa vigumu kuhudumia familia zao katika wakati bei za bidhaa zinaendelea kupanda mjini Juba na kwengineko nchini humo.
"Chakula ni ghali na watoto wanatutia kishindo kwa ajili ya ada za shule" amesema Tereza Akol anayefanya kazi kama karani katika ofisi moja ya serikali huku akisisitiza "Hali yetu ni mbaya."
Akol anasema hajapokea mshahara tangu mwezi Januari mwaka huu. Mary Poni anayefanya kazi ya usafi katika ofisi ya serikali amesema hivi sasa anacho kibarua cha pembeni cha kuuza mbogamboga ili kupata fedha ya kujikimu. "Unawezaje kuihudumia serikali ambayo haikujali?" ameuliza
Mwaka uliopita rais Salva Kiir aliiagiza wizara ya fedha kutenga mapipa 5,000 ya mafuta yanayouzwa kila siku kama chanzo cha mapato ya kulipa mishahara ya watumishi. Hata hivyo hadi sasa hilo halijatekelezwa.