1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan mbili zaanza mazungumzo ya amani

18 Julai 2012

Kabla ya tarehe 2 Agosti, viongozi wa Sudan na Sudan Kusini wamekutana ana kwa ana mwishoni mwa juma, baada ya ukimya wa muda mrefu.

https://p.dw.com/p/15ZNw
Ni rais wa Taifa Jipya Sudan Kusini, Salva Kiir.
Ni rais wa Taifa Jipya Sudan Kusini, Salva Kiir.Picha: picture-alliance/dpa

Viongozi hao wawili hasimu wamekutana Jumamosi, mazungumzo ya kwanza tangu kutokea kwa machafuko mwishoni mwa mwezi April. Lakini wachambuzi wa mambo wanaona mazungumzo hayo bado hayana mashiko.

Siku ya Jumatatu, waangalizi mjini Washington, Marekani walionya kuwa muundo wa mazungumzo hayo bado ni finyu, unaotoa mwanya wa kutokuwepo mapatano kama ilivyoshuhudiwa kwa miaka mingi. Msiuguano baina ya mataifa hayo mawili jirani bado haujatafutiwa ufumbuzi wa kudumu juu ya masuala nyeti yahusuyo utawala mjini Khartoum na maeneo mengine yasiyopewa kipaumbele.

Akizungumza katika jopo la wataalam mjini Washington Jumatatu hii, mwanaharakati mmoja aliyezaliwa Darfur, Omar Ismail, amesema mapatano yanaweza yakafikiwa kwa sababu serikali ya Sudan inahusika. Ameongeza kusema kuwa, hatahivyo, hilo halitasaidia matatizo yanayozikabili Sudan hizo mbili ambapo mojawapo inajitahidi kuwa na demokrasia thabiti, wakati nyingine ikipania kuwa na msimamo mkali usioyumbishwa.

Ni rais wa Sudan, Omar al- Bashir.
Ni rais wa Sudan, Omar al- Bashir.Picha: Reuters

Jumamosi, muda mfupi tu baada ya Sudan Kusini kusherehekea mwaka mmoja wa uhuru wake, marais Omar al- Bashir na Salva Kiir walikutana mjini Addis Ababa kando mwa mkutano wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika, AU, baada ya wote wawili kuhutubia mkutano huo.

Hakuna anayejua kilichozungumzwa na Bashir na Kiir

Wakati wengi hawajui ni nini kilichozungumzwa katika mkutano huo wa Bashir na Kiir, taarifa ya habari zinaeleza kwamba viongozi hao walionekana wakitabasamu na kupeana mikono. Kwa macho ya mtu wa kawaida, picha hiyo inatoa faraja.

Tayari Sudan Kusini imeshasitisha uzalishaji  wa mafuta mwezi Januari, hatua iliyoathiri vikubwa mapato ya serikali zote mbili.

Uhusiano huo mbaya umetiwa doa zaidi na tuhuma kuwa Sudan Kusini inayasaidia makundi ya waasi yaliyopo maeneo kadhaa nchini Sudan. Na serikali mjini Kahartoum nayo inatuhumiwa kwa kuchochea mashambilio dhidi ya raia, na hivyo kusababisha maelfu ya wakimbizi kuingia Sudan Kusini katika miezi ya hivi karibuni. Matokeo yake ni kuidhoofisha serikali mpya ya Juba na juhudi pia za kimataifa kuhusiana na ustawi wa binaadamu.

Mkutano wa Jumamosi mjini Addis Ababa, Ethiopia, ulifanyika siki hiyo hiyo ambapo taarifa rasmi ya Umoja wa Afrika ilitolewa ikielezea jinsi maendeleo ya kuumaliza mgogoro wa nchi hizo mbili yanavyozorota, huku zikiwa zimebakia siku chache kabla ya muda wa mwisho uliowekwa na Umoja wa Mataifa kumalizika.

Tarehe 2 Agosti ndiyo tarehe iliyowekwa na kuridhiwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo ikiwa pande hizo zimeshindwa kufikia mapatano juu ya changamoto zake, basi vikwazo vitatekelezwa Sudan na Sudan Kusini.

Muasi katika eneo la machafuko huko mpakani mwa Sudan hizi mbili.
Muasi katika eneo la machafuko huko mpakani mwa Sudan hizi mbili.Picha: Reuters

Pagan Amum anasemaje kuhusu mgogoro huu?

Vyombo vya habari vilimnukuu mpatanishi mkuu wa Rais Kiir, ambaye pia ni katibu Mkuu wa chama tawala cha Sudan People´s Liberation Movement, (SPLM), Pagan Amum, akisema kuwa viongozi hao wawili wamezielekeza timu zao za upatanishi namna ya kuharakisha mazungumzo hayo ili kuumaliza mzozo kati yao.

Wiki za hivi karibuni, kumeshuhudiwa maandamano ya umma nchini Sudan, raia wakilalamikia kile walichokiita matatizo ya kiuchumi, hali ambayo Omari Ismail anasema imesababishwa na serikali yenyewe.

Raia huyu anasema raia wa taifa hili wanahitaji kuishi kwa amani, iwapo kama kutakuwa na utulivu Sudan hata nchi jirani zitakuwa na amani.

Aliyekuwa mwanadiplomasia wa Sudan ambaye sasa ni mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa, anayeshughulikia kuepusha mauaji ya halaiki, Francis Deng, anasema kushindwa kuyatatua matatizo yanayoikabili Sudan Kusini ndiyo chanzo kilichodumu kwa miaka nenda rudi na hatimaye kusababisha mabadiliko ya uongozi mjini Khartoum.

Mwandishi: Pendo Paul

Mhariri: Miraji Othman