Sudan na Sudan Kusini wafikia makubaliano
12 Machi 2013Kulingana na Makubaliano hayo yaliotiwa saini katika mji mkuu wa Ethiopia Addis, nchi hizo mbili Sudan na Sudan Kusini zina siku 14 za kuamrisha kampuni za mafuta katika maeneo hayo kuanzisha tena uzalishaji wa bidhaa hiyo.
Rais wa zamani wa Afrika Kusini ambaye ndiye mpatanishi mkuu wa mzozo kati ya nchi hizo Thabo Mbeki, amesema kampuni za mafuta tayari zimeagizwa kuanza kufanya kazi tangu tarehe 10 mwezi huu lakini bado zina muda wa wiki mbili kutekelezwa agizo hilo.
Idris Mohammed Abdel Gadir, Kiongozi wa ujumbe wa Sudan alitia saini makubaliano hayo na mwenzake wa Sudan Kusini Pagan Amum hatua inayotoa nafasi ya biashara hiyo ya mafuta kuanzishwa upya. Hii imefanyika baada ya siku nne za mazungumzo yalioanzishwa na Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia.
"Pande mbili za sudan na sudan kusini leo asubuhi wametia saini makubaliano ambayo yametokana na makubaliano ya septemba mwaka wa 2012 , kwa hiyo makubaliano hayo yanajumuisha ushirikiano wa nchi hizo mbili katika usalama na uchumi," Alisema Bader El Din Abdullah, msemaji wa ujumbe wa Sudan.
Sudan na Sudan kusini hutegemea sana pato la bishara ya mafuta na kutumia fedha za kigeni kuingiza bidhaa ya mafuta na chakula, lakini kutokana na mzozo wa mpakani na masuala mengine, yalizizuia nchi hizo kuendeleza biashara zao.
Ugomvi wa Sudan na Khartoum
Sudan Kusini iliacha kuchimba mafuta mwaka jana kwa sababu ya ugomvi wake na Khartoum kuhusu kiasi gani inafaa kuilipa Sudan kwa kusafirisha mafuta yake kwa kutumia miundo mbinu ya Sudan, na hata kumshitumu jirani yakekwa wizi wa mafuta yake.
Wakati huo huo majeshi ya nchi hizo pia yamekubaliana kuanza kuondoa vikosi vyao katika mpaka kumbewa, katika muda wa wiki moja. Hata hivyo wataalamu na wachambuzi wa kisiasa wanasema hawana matumaini ya jambo hilo kufanyika.
Jumatatu iliopita Sudan ilitangaza kuwa vikosi vyake vilishambuliana na kundi la waasi la SPLM-N katika jimbo la Blue Nile. Sudan inaishutumu moja kwa moja Sudan Kusini kwa kuwaunga mkono waasi hao katika vita vya mwaka wa 1983 hadi mwaka wa 2005 jambo ambalo limekuwa changamoto kubwa katika kufikia makubaliano ya amani kati ya nchi hizo mbili.
Mwandishi: Amina Abubakar/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman