Sudan yafuzu kwa robo fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika
31 Januari 2012Mudather Tyeb aliifungia Sudan magoli yote mawili katika uga wa Estadio be Bata na kuinyanyua soka ya nchi hiyo juu tangu iliposhinda kombe la Afrika katika ardhi ya nyumbani mnamo mwaka 1970. Pia ulikuwa ushindi wa kwanza wa Sudan katika kinyang'anyiro hicho tangu ilipotwaa kombe hilo.
Mudather alimbwaga kipa wa Burkinabe Daouda Diakite katika dakika ya 33 na kisha akmwadhibu kipa baada ya kufanya masihara katika kipindi cha pili na kuikatia tiketi Sudan licha ya Burkina Faso kufunga bao zikiwa zimesalia dakika saba mchuano kukamilika.
Angola ambayo ilihitaji tu pointi moja kutoka kwa mchuano wake wa mwisho ili kufuzu, ilishindwa mabao mawili kwa nunge na Cote d'Ivoire ambayo ilikuwa tayari imefuzu, na hivyo ikaisalimisha nafasi ya pili kwa Sudan na kubanduliwa nje baada ya kufungwa bao jingine katika awamu ya makundi.
Tofauti ya mabao ndiyo iliyoamua baada ya Sudan na Angola kutoka sare ya magoli mawili katika mchuano wao wa makundi. Sudan sasa itakabana koo na mshindi wa kundi A Zambia, huku Cote d'Ivoire inayopigiwa upatu na wengi ikikutana na mwenyeji Guinea ya Ikweta katika mcehi za robo fainali.
Kikosi cha Sudan kinazidi kuimarika
Kocha wa Sudan Mohammed ‘Mazda' Abdullah alifurahishwa na ushindi huo akisema walihitaji kuwa katika robo fainali. Alisema vijana wake walicheza vyema, na kwamba kikosi chake kina wachezaji chipukizi kikiwa na umri wa wastani wa miaka 24. Mazda alisema mchuano huo ndio uliokuwa wao bora zaidi.
Naye mwenzake wa Burkina Faso Paulo Duarte alisema timu yake ina maisha mema katika siku zijazo. Alisema ikiwa atasalia kama kocha wa timu hiyo, basi watafuzu kwa mechi za kombe la dunia, kwa sababu wana uwezo wa kufanya hivyo.
Mjini Malabo Mabao ya Cote d'Ivoire yalifungwa na beki wa zamani wa Arsenal Emmanuel Eboue na Wilfried Bony. Kocha wa The Elephants jinsi wanavyofahamika Francois Zahoui aliridhika kuwaona vijana wake wakiendelea vyema katika dimba hilo. Alisema afueni kamili itakuwa kushinda taji hili.
Alisema ataridhika ikiwa watatimiza lengo lao la kuwafurahisha watu wa Cote d'Ivoire. Naye kocha wa Angola, Lito Vidigal, alisema mchuano ulikuwa mgumu na kwamba walijizatti vilivyo. Aliongeza kuwa walikuwa na matatizo mengi wakati wa kufuzu kwa fainali hizo za kombe la afrika, lakini akawashukuru mashabiki.
Mechi za kundi C kuchezwa hii leo
Hii leo wenyeji Gabon na Tunisia wataumiza nyasi katika mchuano wa mwisho wa kundi C. timu zote mbili tayari zimefuzu kwa awamu ya nane za mwisho katika kivumbo hicho baada ya kushinda michuano yao ya kwanza mbili. Mechi hiyo basi litaamua ni nani atakayeongoza kundi hili ili kurejea katika mji mkuu wa Gabon Libreville kwa mchuano war obo fainali dhidi ya timu nambari mbili ya kundi D.
Gabon ilionesha mchezo bora baada ya kutoka nyuma bao moja na kuwazaba Morocco mabao matatu kwa mawili katika mchuano wao wa mwisho wa makundi mjini Libreville. Kocha wa Gabon Mjerumani Genort Rohr, ambaye ameitayarisha timu yake kwa miaka miwili, alisema sio rahisi kutoka nyuma na kusajili ushindi na hiyo inamaanisha timu ni thabiti. Rohr alisema wana matarajio makubwa hata ingawa wao sio mojawapo wa mataifa yanayopigiwa upatu.
Kwa upande wake mwenzake wa Tunisia Sami Trabelsi tayari ana maono ya mbali na mchuano wa Gabon na amedokeza kuwa anapanga kufanya mabadiliko kadhaa kwa kikosi chake kwa sababu wachezaji kadhaa tayari wana kadi za njano na ikiwa watakula tena kadi hii leo watakosa mechi ya robo fainali.
Nambari mbili wa kundi C watasalia mjini Franceville nchini Gabon ili kupambana na washindi wa kundi D, ambalo linajumuisha Ghana, Guinea, Mali na Botswana. Sare kwa wenyeji Gabon itatosha kwa vile tayari wana tofauti kubwa ya magoli kuliko Tunisia. Katika mchuano mwingine wa kundi C ambao hautakuwa na maana yoyote ni kati ya Niger na Morocco ambazo tayari zimeyaaga mashindano hayo. Mechi hii itachezewa mjini Libreville.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef