Sudan yakubali upatanishi wa S.Kusini majimbo ya mpakani
5 Novemba 2018Sudan iliwahi kuilaumu Sudan Kusini kwa kuchochea machafuko katika mikoa hiyo miwili ambako waasi wanapigana dhidi ya utawala wa serikali ya Sudan baada ya sehemu kubwa ya ardhi ya majimbo hayo kuwa sehemu ya Sudan Kusini huru katika mwakan 2011.
Serikali ya Sudan imetangaza usitishaji mapigano wa upande mmoja katika majimbo yote mawili na pia katika jimbo lenye mgogoro la Darfur magharibi mwa Sudan tangu mwaka 2015, na sasa mapigano yamepungua.
Msemaji wa chama tawala nchini Sudan Ibrahim al-Sadiq alisema, rais Salva Kirr wa Sudan Kusini ameanza mazungumzo na makundi ya chama cha Sudan Peoples Liberation Army-SPLM yalioko katika mikoa hiyo miwili kuhusu suluhisho la amani.
Alisema mazungumzo hayo chini ya udhamini kwa udhamini wa Umoja wa Afrika yanatarajiwa kuanza mjini Addis ababa katikati ya mwezi ujao wa Desemba.
"Amani ni chaguo la kimkakati kwa serikali ya Sudan na kwa hivyo serikali imeidhinisha upatanishi wa rais wa Sudan Kusini Salva Kiir," alisema Sadiq.
Maelfu yawatu wameuawa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mataifa ya Sudan, ikiwemo jimboni Darfur, ambako waasi wamekuwa wakipigana dhidi ya serikali ya Rais Omar Hassan al-Bashir tangu mwaka 2003.
Serikali ya Kiir na kundi kuu la waasi wa Sudan Kusini walisaini makubaliano ya amani mwezi Spetemba mjini Khartoum, yakinuwia kukomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoiharibu nchi hiyo tangu mwaka 2013.
Mwandishi: Iddi Ssessanga
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman