Swala la uongozi latawala mkutano wa siku nne wa wajumbe wa chama tawala nchini Afrika Kusini-ANC.
29 Juni 2007Katika mkutano wa siku nne wa wajumbe wa chama hicho swala la uongozi lilitawala mazungumzo yao. Katibu mkuu wa chama hicho Kgalema Motlanthe amewaambia wanahabari kuwa wajumbe hivi leo walijadili mapendekezo kadhaa njisi ya kutatua mzozo wa uongozi uliojitokeza chamani baada ya rais Mbeki kumfuta kazi makamu wake Jacob Zuma. Wengi walimwona Zuma kuwa katika nafasi ya mbele kuchukua nafasi ya rais Mbeki baada ya muhula wake wa pili kukamilika.
Zaidi ya wajumbe 1,500 wanaohudhuria mkutano huo huenda wakafanyia mabadiliko sheria za chama hicho cha ANC na kuondoa utaratibu ambao umekuwepo tangu mwaka wa 1994 ambapo kiongozi wa chama anakuwa moja moja mgombezi wa urais wa chama hicho.
Iwapo sheria hiyo itapitishwa Rais mbeki huenda akapoteza nafasi ya kuwa kiongozi wa chama hicho baada ya kungatuka mamlakani na kumpisha mpinzani wake Jacob Zuma. Hata hiyo chama hicho cha ANC kitalazimika kubadilisha katiba yake iwapo kitamzuia Rais Mbeki kuwa kiongozi wake.
Rais Mbeki hajafuta uwezekano wa kugombea tena kiti cha urais kwa muhula wa tatu kwa chama hicho cha National African Congress japokuwa katiba ya Afrika Kusini inamzuia kuendelea kuliongoza taifa hilo baada ya mwaka 2009.
Na si wajumbe tu wanaliohudhuria mkutano huo bali pia wataalam wa maswala mbalimbali ambao wanajadili kuhusu mwelekeo na utendaji wa chama hicho serikalini.Sera walizozungumzia zinajumuisha maswala ya uchumi, utawala na mfumo wa sheria ya uhalifu.
Katika mkutano huo Serikali imehitajika kuangalia pia kuhusu njia ya kufanyia mageuzi uchumi wa afrika kusini ili kuhakikisha ushiriki zaidi wa watu wa kawaida kwani viwango ambayo si rasmi vya watu wasikuokuwa na ajira ni zaidi ya asilimia 40.
Mkutano huo wa chama cha National African Congress unafanywa mjini Midrand karibu na Johannesburg.