Tahadhari yatolewa kote India baada ya mashambulizi ya mabomu
27 Julai 2008AHMEDABAD
Miji mikuu nchini India imetakiwa kuchukua tahadhari baada ya kutokea mlolongo wa mashambulio ya mabomu magharibi mwa mji wa Ahmedabad ambapo watu 45 waliuwawa na wengine kiasi cha 145 wakajeruhiwa hapo jana.
Polisi leo wamegundua mabomu mengine zaidi ambayo hayajalipuka.Serikali ya India imetoa amri maduka yafungwe na watu wabakie majumbani.
Wakati huohuo polisi wamevamia nyumba mmoja karibu mji wa kibiashara wa Mumbai katika harakati za kuwasaka wahusika wa mashambulio hayo.
Maafisa hao wamekamata computa ambayo ilitumiwa katika kutuma barua pepe inayodai juu ya kundi lililokuwa na dhamana ya mashambulio hayo.
Vyombo vya habari nchini India vimeripoti kuwa kundi dogo lisilofahamika sana linalojita Mujahedeen wa India limedai kuhusika na mashambulio 16 yaliyoutikisa mji wa Ahmedabad hapo jana.
Mfululizo huo wa mashambulio ya mabomu ulifuatia mashambulio mengine kusini mwa mji wa Bangalore siku ya ijumaa.