1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Takriban 100 wafariki, mamia wakwama mgodini Afrika Kusini

Bryson Bichwa
14 Januari 2025

Zaidi ya wachimba migodi haramu 26 wameokolewa na karibu miili kumi kuondolewa kwenye mgodi uliotelekezwa nchini Afrika Kusini. Operesheni za uokozi zilianza tena Jumanne kuwafikia watu zaidi waliokamwa mgodini hapo.

https://p.dw.com/p/4p8ln
Südafrika | illegaler Bergbau in Stilfontein
Picha: Emmanuel Croset/AFP

Takriban watu 100 wameripotiwa kufariki dunia baada ya kukwama kwa miezi kadhaa katika mgodi wa dhahabu uliotelekezwa kaskazini magharibi mwa Afrika Kusini, ambako walikuwa wakichimba madini kinyume cha sheria.

Mgodi huo wa Stilfontein, uliopo katika eneo la kaskazini magharibi mwa nchi, umegeuka kuwa chanzo cha maafa makubwa, huku juhudi za kuwaokoa wachimbaji waliobaki zikiendelea chini ya usimamizi wa Wizara ya Nishati na Madini.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya wachimbaji haramu 500 bado wako ndani ya mgodi huo. Zoezi la kuwatoa limeanza rasmi, lakini hali ya wasiwasi imeongezeka kwa familia za waliokwama mgodini, zikisubiri kwa hofu habari za wapendwa wao.

Familia za wachimbaji katika hali ya kukata tamaa

Maggie Mutabi ni mmoja wa wachimbaji waliokwama mgodini, ambaye aliondoka nyumbani miezi sita iliyopita akiwa na matarajio ya kurudi baada ya miezi mitatu. Familia yake sasa iko katika hali ya kukata tamaa huku kukiwa na uhaba wa chakula na hofu ya kupoteza mpendwa wao.

Soma pia: Familia za wachimbaji Afrika Kusini zasubiri hatma za wapendwa wao

"Hivi tunavyozungumza hatuna chochote, hatuna chakula, na tunayemtegemea yuko mgodini. Hatuna uhakika kama bado yu hai, maana wanasema watu wengi wamekufa," alisema Mutabi kwa uchungu.

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa
Rais wa Afrika Kusini Cyril RamaphosaPicha: Themba Hadebe/AP/picture alliance

Picha za kutisha za miili ya wachimbaji waliokufa zilianza kusambaa mitandaoni mwishoni mwa juma lililopita. Inaripotiwa kuwa zaidi ya wachimbaji 100 wamefariki dunia baada ya polisi kuzuia chakula, maji, na dawa kuingia mgodini, kwa lengo la kuwashinikiza wachimbaji haramu kujisalimisha na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mashuhuda wasema idadi ya vifo ni kubwa zaidi

Kwa mujibu wa Sabelo Mnguni, afisa mkuu wa jamii zilizoathiriwa na uchimbaji wa madini, idadi ya waliokufa huenda ikawa zaidi ya 100.

"Watu wa kujitolea walioshuka mgodini wanasema kuna miili mingi kuliko ile iliyoonekana kwenye video zinazosambaa. Kamera hazikunasa maeneo yote ambayo miili hiyo iko. Kumbuka, chini ya ardhi kuna ngazi zaidi ya tano, na mashuhuda wetu wanasema kila ngazi ina takriban miili 70 au zaidi ya waliokufa," alisema Mnguni.

Soma pia: Wachimba mgodi 955 waliokwama Afrika Kusini waokolewa

Liva Belosi, kiongozi katika eneo la Bluefotain ambako mgodi huo upo, ameishutumu serikali kwa kupuuza suala hilo na kuwatelekeza wachimbaji hao. Belosi ametaka Waziri wa Nishati na Madini pamoja na Waziri wa Polisi wawajibishwe kutokana na vifo hivyo.

"Hii si serikali ya watu. Tunataka kutuma ujumbe wa wazi kwa Waziri wa Madini na Waziri wa Polisi kwamba lazima wawajibike kwa vifo hivi," alisema Belosi kwa hasira.

Wachimba migodi wanusurika Afrika Kusini

Zoezi la uokoaji linaloendelea

Kundi linalowawakilisha wachimbaji hao limesema kuwa miili 18 na manusura 26 wametolewa kutoka mgodi wa Stilfontein tangu Ijumaa iliyopita. Hata hivyo, zaidi ya wachimbaji 500 bado wanaaminika kuwa wamekwama chini ya ardhi. Polisi wanasema hawana uhakika kamili wa idadi ya waliobaki mgodini, lakini wanakadiria kuwa huenda wakawa mamia.

Huku zoezi la uokoaji likiendelea, mashirika ya haki za binadamu yameitaka serikali ya Afrika Kusini kuchukua hatua za haraka ili kuhakikisha kuwa maisha ya wachimbaji waliobaki yanahifadhiwa, na kufanya uchunguzi juu ya mazingira yaliyosababisha janga hili.